Uchambuzi Wetu: Matumizi ya Simu Miaka ya Baadae

 

Simu ni kifaa kilichopata mabadiliko ya haraka, ningali naikumbuka Nokia Ringo na Motorola Startec, simu za mwanzoni kabisa kuingia Tanzania wakati wa enzi za Mobitel. Ukifananisha simu zile na hata simu ambayo leo tunaiona kuwa ni kimeo, basi utakubali kuwa simu ni kifaa kilichobadilika mno na tena kwa haraka sana. Katika makala hii tunajaribu kuangalia mbele, ni vipi tutaitumia simu katika maisha yetu hapo baadae. Ni vigumu kuwa sahihi kwa asilimia mia moja, lakini tunaamini haya tutakayoyaelezea yatatokea. Kutokana na teknolojia mbali mbali kuingizwa kwenye simu, teknolojia kama vile Gyroscope, Near Field Communication (NFC), GPS, Digital Compass, Accelerometer na sensa nyingine mbali mbali simu itakuwa ni kifaa chenye matumizi ya ajabu kabisa, mbali na kuwa itatumika kiajabu. Yafutayo ni baadhi tu ya mambo ambayo simu itakuwa inauwezo wa kuyafanya miaka michache ijayo, yaani tunazungumzia chini ya miaka kumi hivi.

Simu kama pesa: itachukua nafasi ya kadi za benki, teknolojia ya NFC inaipa nafasi kubwa sana simu kufanya hili, tayari teknolojia hii imeshaanza kutumika, kwa mfano kampuni ya Orange hukubali malipo ya chini ya £15.00 nchini Uingereza kwa kutmia simu zao, ambazo zimeingizwa taarifa za kadi yako ya benki. Nchini Marekani Google wameanzisha huduma waliyoiita Google Wallet, ambayo nayo inakuwezesha kufanya mali[po kwa kutumia simu.
Kitambulisho: Simu kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi data, inaweza kuwa ni kitambulisho chako, kwa vile inauwezo wa kuhifadhi finger print au taarifa nyingine zozote za ‘artificial intellingence’. Kwa hiyo simu inaweza kuwa leseni au hata pasipoti. Sitoshaangaa baada ya miaka kadha mtu asafiri na simu badala ya pasipoti na ticket.
Funguo za Gari: Tayari BMW na kampuni nyingine wameshatoa gari ambayo inafunguliwa kwa Fob, teknolojia hii inaweza kuingizwa kwenye simu, tayari kuna gari ambazo zinawashwa na iPhone 4, kama vile BMW x5 zilizotoka kuania mwaka 2010. 
Funguo za Milango: Teknolojia ya Fob inaweza na tayari inatumika kufungulia milango kwa hiyo hili nalo linawezekana na si mud amrefu watu watafungual milango ya nyumbani au kazini kwa kutumia simu zao.
Box la TV: Simu tayari ina uwezo wa kuwa mbadala ya DVD, muda si mferu itakuwa ni mbadala wa box la TV (Set top Box), tayari HTC Flyer ikitumia huduma ya streaming wanakodisha movies kwenye tablet hii, bila ya shaka huduma hii itakuwepo kwenye simu za HTC zijazo, nchini Uingereza  Skysports wanaonyesha mechi za La Liga na Primier League kwenye iPhone kwa gharama za £8.00 kwa mwezi. Ninazungumzia mechi kama zinavyojiri (live stremaing), weka na huduma ya iCloud bial ya shaka huko mbele mambo yatakuwa moto.
Game Console: tutakuwa hatuhitaji PS3 wala PS10, ni simu tu. Mwezi wa tisa Real Race itakuwa ni game ya kwanza kutoka kwenye iPhone kwa msaada wa Apple TV itaonesha kwenye TV moja kwa moja na hivyo iPhone itakuwa ni kontrola tu.
Simu kama Daktari: Tayari iPhone inaweza kutumika kama kifaa cha kupimia BP, muda si mrefu simu zitakuwa ni kama kifaa cha kidaktari kufanya mambo kama kuchukua vipimo kwa joto la mwili, BP, sukari ya mwili na vipimo viengine. Vile vile Chuo Kiku cha Carlifnia tayari kimo mbioni kutengeneza kifaa cha kupimia Malaria kitakachotumika kwenye simu.

Kamera na Kamkoda: Ingawa kwa sasa simu zina kamera na kamkoda bado watu wanaendelea kuona umuhimu wa kuwa na vifaa hivyo kwa vile tu teknolijia hizi bado zimo njiani kuboreka kuelekea kwenye kiwango cha kitaalam au cha hali ya juu kinachopatikana kwenye gajeti hizi. Si muda mrefu hatutahitaji tena kuwa na kamkoda au kamera kama vifaa pekee bali simu itatosheleza mahitaji haya, kwa upande wa kamera watu wenye simu kama vile iPhone 4, Samsung Galaxy S 2 na HTC Evo 3D hawaoni tena umuhimu wa kuwa na kamera.

Kwenye makala zijato tutajaribu kuangalia simu za baadae zitakuwa vipi kimaumbile na kutumiaka namna gani, kwa sasa ni kibodi, skrini za kugusa, amri za sauti (voice command) na kadhalika. Ni vipi simu zatatumika baadae? Endelea kutembelea tovuti hii.

Uchambuzi Wetu: Blackberry Bridge

 

Research In Motion, watengenezaji wa simu za blackberry bado hawako nyuma katika uvumbuzi na uboreshaji wa bidhaa zao mbali mbali. Mwaka huu RIM wametoa tablet yao ya kwanza, Blackberry Playbook, katika tablet hii wamekuja na kile walichokiita Blackberry Bridge, huduma hii inaunganisha simu yoyote ya Blackberry inayotumia Blackberry OS toleo la 4 kwenda mbele na BB Playbook, unapounganisha tablet na simu ya Blackberry kwa njia ya Bluetooth na kupitia app ya BB Bridge unapata faida za kutumia internet ya simu yako kwenye Playbook kupitia Bridge Browser (tethering), pia inakuruhusu kutumia apps za Messeges, Contacts, Calender, BBM, Memopad, Tasks na Bridge Files.
Uchambuzi Wetu utajaribu kuangalia manufaa na hasara ya huduma hii ya kipekee waliokuja nayo RIM katika Blackberry Playbook. Kabla hatujaingia katika uchambuzi ni muhimu tufahamu kwamba ikondoa Browser, apps zote nyingine ambazo zimo kwenye Bridge hazipatikani kwenye Playbook bila kufanya bridge. ukiangalia umuhimu wa apps hizo, hii ina maana kwamba Playbook inakaribia kuwa haina maana bila ya kuwa na simu ya Blackberry. Tukianza na uchambuzi, bila ya shaka RIM wamefanya hivi ili kuwalazimishsa watakaonunua Playbook kununua pia simu ya Blackberry. Kwa hiyo kama wewe ni mtumiaji wa simu za Android, iPhone au Windows Phone, fikiria mara mbili kabla ya kununua Blackberry Playbook.
Wakati Playbook haitumii 3G au 4G kwa sasa, kwa maana ya kwamba haiingii kadi ya sim, lilikuwa ni wazo sahihi kabisa kuweka Bridge Browser ili kunufaika na internet ya simu pale ambapo uko pahala usipoweza kupata WiFi. Hapa RIM wamecheza kama Pele. Ni ugunduzi mzuri tena wenye manufaa kwa kiasi kikubwa, kwa vile tumefika mahala ambapo tunajiuliza tutakuwa na gajeti zenye kadi za sim ngapi, simu inatumia kadi hiyo, ongeza tablet, ongeza na game (PS Vita  pia itakuwa na sim) na hivyo kuwa na bili chungu nzima. Kwa hiyo RIM wametuepushia kulipia internet za 3G mara zaidi ya moja baina ya tablet na simu.
Wakati Bridge ni wazo zuri, kutoweka kabisa apps hizi kwenye Playbook kunaifanya Playbook kupungua maana kwa watumiaji wa simu ambazo si Blackberry. Kwa upande wa watumiaji wa Blackberry, baada ya kuijaribu huduma hii tumegundua kwamba baadhi ya wakati huwa apps hizi hazifanya kazi kwa ufanisi, huwa zina kasi isiyoridhisha, huenda hili linasababishwa na ukweli kwamba Playbook na Simu ya BB huunganishwa kwa teknolojia ya bluetooth. wengi tunafahamu kuwa mawasiliano kwa njia hii si yenye kasi kubwa. 
Playbook itabaki kuwa mfungwa wa simu za BB mpaka RIM watakapotimiza ahadi ya kuweka apps muhimu zilizo kwenye BB Bridge
Afisa Mtendaji Mkuu mwenza wa RIM, Mike Lazaridis  ameahidi kuwa RIM wataweka apps hizi kwenye Playbook watakapofanya uboreshwaji wa OS yake, mpaka ahadi hii itakapotimia, hili linabaki kuwa ni kasoro ya kukosa apps muhimu kabisa, yaani ni jambo ambalo si la kufikirika katika Ulimwengu wa leo kuwa una tablet lakini huwezi huna contacts au inabidi email uangalie kwenye browser ya kawaida badala ya app maalum.

Simu Kupima Malaria

 

Wataalam katika Chuo Kikuu cha Carlifonia wamo katika harakati za kutengeneza chip ambayo itawekwa kwenye simu na kuwa na uwezo ya kugundua vijidudu vya Malaria kwenye mwili wa binadamu. Wanasayansi wawili wa Chuo hicho Peter Lilhoj na Chih-Ming Ho tayari wameshapata ruhusa ya kutengeneza kifaa hicho kutoka kwenye vyombo husika. Kifaa hicho kitakuwa kinatumika mara moja na kutupwa (disposable) na hivyo bila ya shaka kitakuwa ni kifaa cha kuchomeka tu badala ya kutengenezwa ndani ya simu. Kitakuwa kinafanana na kadi ya sim, kwa hiyo ni watumaini yetu kuwa kitatumika kwenye nafasi ya kadi kwa maana ya kwamba hakutakuwa na simu maalum yenye kufanya kazi hii, bali ni simu zote.

Wakati wametuacha bado tukitafakari ni vipi simu itapima na kugundua kilichopo kwenye damu, wataalam hao wameeleza kuwa lengo  la mradi huu ni kurahisisha na kusambaza upimaji na ugunduaji mapema wa maradhi haya ambayo mpaka sasa yameshateketeza maisha wa watu wengi mno Duniani na hasa katika nchi zilizoko Amerika ya Kusini, Afrika na Bara Hindi. Mradi huu unategemea kuanza kutumika nchini Msumbiji katika maeneo ya vijijini mara tu baada ya kukamilika kwa utengenezajiwa kifaa hichi. Bila shaka hii italeta faraja kubwa katika kuigundua Malaria hata hivyo matibabu hayatabadilika. Chuo Kikuu cha Carlifonia hakikuthibitisha ni lini kifaa hichi kitakuwa tayari kutumika.

Hacker Geohot Aajiriwa na Facebook

 

Geohot, hacker maarufu aliyejailbrake iPhone ameajiriwa rasmi na Mark Zuckerburg, yaani Facebook. Hacker huyu ambaye pia aliwahi kushitakiwa na Sony kwa shughuli za uchakachuaji baada ya kuihack PS3 na kuruhusu watumiaji kuweza kutumia DVD feki za kuchakachua. Facebook hawakuthubitisha Geohot atafanya kazi gani kwenye kampuni hiyo. Hacker huyu ambaye anatumia majina mbali mbali katika shughuli zake pevu ikiwa ni pamoja na million75, mil, dream na hax0r ameshafanya fujo nyingi sana katika ulimwengu wa kompyuta. Kijana huyu kwa sasa ana umri wa miaka 22 tu.

Jina alilopewa na wazazi wake ni George Francis Hotz. Katika kazi za karibuni kabisa alizofanya hacker huyu ni kujailbraik iPhone na iPod Touch kwa kutumia njia aliyoiita Blackra1n na pia kuifungua (sim unlock) simu hiyo kwa njia aliyooiita blacksn0w.
Alipoihack PS3 Sony walimpandisha kizimbani, hata hivyo mwezi wa nne mwaka huu Sony na Geohot walikubaliana nje ya mahakama na hivyo Sony kufuta kesi ile. Geohot alipewa sharti la kuto-hack tena PS3 ili kufutiwa kesi hiyo, sharti ambalo alilikubali. Ajira hii kwa dogo huyu ni hasara kubwa kwa wachakachuaji kwani watakosa mengi pale atakapotingwa na kazi za Facebook. Hacker huyu huwa hana noma, baada ya kufanya mambo yake huyaweka wazi kabisa katika tovuti yake ambayo ni www.geohot.com 
Kwa sasa kwenye tovuti yake ameacha ujumbe mfupi wa ajabu, waweza kwenda kuangalia mwenyewe.

Matumizi 10 ya simu na Tablet

 

Steve Jobs, Afisa Mtendaji Mkuu wa Apple akizungumza katika uzinduzi wa iPad alisema tunaanza kuishi katika kipindi ambacho kompyuta (akimaanisha desktop na laptop) imeanza kupitwa na wakati (post computer era). Ingawa tablet si aina mpya ya kompyuta, lakini iPad imeleta mabadiliko makubwa juu ya vipi tablet iwe na itumike. Mwaka huu ikiwa tumeugawa nusu, tayari kuna tablet zaidi ya 100 mpya zilizotolewa na kampuni mbali mbali, zipo za rahisi kabisa kama ile iliyotolewa India ambayo inagharimu $25.00 tu, na pia zipo za ghali mno kama ile ya iPad ya dhahabu na almasi ambayo imeuzwa Mamilioni ya dola.  Zipo zenye maudhi kwa kukosa ufanisi na pia zipo zenye maajabu kutokana na ufanisi wa hali ya juu kabisa.  Kwa upande wa simu, katika miaka ya karibuni kumetokea mapinduzi makubwa ya simu kutokana na ushindani wa kibiashara, simu imekuwa na uwezo, kasi na utendaji karibu sawa na kompyuta. Kiujumla matumizi ya simu na tablet yanafanana sana, lakini pia kuna tofauti mbili za msingi. Awali tablet si simu na pili simu huwa na display ndogo. Haya ni baadhi tu ya matumizi ya gajeti hizi:-


1. Mawasiliano

Hii ndio kazi ya msingi kabisa. Simu ni kifaa cha mawasiliano, hufanya shughuli kama vile kupiga simu, kuandika na kusoma meseji, kusoma email na mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter na My Space, kwa upande wa simu, hili ni maarufu zaidi kwa watumiaji wa Blackberry ambapo wengi tayari ni wagonjwa (addicted) katika matumizi ya Blackberry Messenger (BBM). Huduma kama hizi zinaonekana kutanuka zaidi ambapo iPhone nayo inategemewa kuanza huduma za iMessage miezi michache ijayo. Hata hivyo tablet inaonekana kuwa ni kifaa bora zaidi kwa kusoma mitandao jamii wakati simu ni bora zaidi kwa kuchangia kwa vile wengi wana kasi ya kuandika katika simu kuliko tablet.

2. Games
Simu hutumika kuchezea michezo (games) mbali mbali kama vile Angry Birds na Neeed For Speed. Kutumia games kwenye simu kumeongezeka zaidi katika miaka minne iliyopita hasa baada ya iPhone na Android kuingia kwa nguvu zote katika uwanja huu. Watabiri wengi wa mambo ya gajeti wanauona Ulimwengu wa baadae katika games kuwa upo kwenye tableti na simu za mkononi. Kwa upande wa tablet games nazo zinashamiri kwa kasi ya ajabu. Kwa mfano tablet yenye uhaba mkubwa wa apps, Blackberry Playbook imetoka ikiwa tayari ina game maarufu ya magari Need For Speed. Kampuni kubwa za games kama vile EA Sports na Unreal Technology wanashiriki kikamilifu katika kutoa games katika vifaa hivi. Cha kufurahisha zaidi ni kwamba games katika platfomu ya tablet na simu zinauzwa bei rahisi mno kulinganisha na Konsoli kama vile PS3 na Wii.

3. Msaidizi
Simu hutumika kama sekretari wa digital yaani kukukumbusha mambo mbali mbali, ikiwemo miadi (reminders), kazi mbali mbali (tasks), memo na mambo kama haya. Simu imekuwa ni kifaa maarufu cha kuamsha wale wenye kuamka mapema kwa sababu za kikazi au sababu nyingine. Hapa simu na hata tablet huonekana kama muokozi na msaidizi mkubwa katika maisha muhimu badala ya kifaa cha kujiburudiashia na mawasiliano tu.

4. Kusoma vitabu
Ingawa hili bado sio maarufu sana, wengine hutumia simu zao kusomea vitabu (ebooks) na hasa watumiaji wa iOS na Android. Hii imeletwa na iPhone pale walipoingiza app ya iBooks. Tablet kwa upande mwingine inaonekana kuwa ndio kifaa sahihi kabisa kwa shughuli za kusomea vitabu, kiasi kwamba soko la ebook readers limeingia mashakani mno kwa vile tablet mbali ya kusomea vitabu ina kazi nyingi zaidi. Hata hivyo kwa wale wenye kujali afya za macho yao wameendelea kutumia ebook reader kwa kusomea vitabu kwa vile diplay za ebook readers kama vile Kindle na Kobo hazina mwangaza.

5. Video calling
Hii ni huduma ambayo zaidi inategemea mtandao. Ingawa wengi wanadhani kwamba badi haiatumika ipasavyo tayari ipo katika platfomu mbali mbali kama vile iOS, Windows, Blackberry na Android. Huduma hii bado inatarajiwa kukua zaidi hapo miaka ya baadae. Huduma maarufu zaidi katika Vidoe calling ni Skype.

6. Kutembelea Tovuti
Hili kimsingi ni lenye kuvutia wengi zaidi, ambapo kampuni nyingi hasa katika nchi nilizoendelea zimekuwa zikiwabana watumiaji kwa kuwawekea kiwango maalum kinachoruhusiwa, kwa sasa wengi huruhusu baina ya 500 MB mpaka 1 GB kwa mwezi. Si kwenye tablet wala kwenye simu wengi wamekuwa wakitumia mtandao katika vifaa vyao, wengine hata bila ya kujali gharama.

7. Multimedia
Kupiga picha, kuzihifadhi, kurekodi video na kusikiliza muziki ni seheme ya maisha ya mwanadamu katika matumizi ya simu na tablet. Wengine hata wamefikia hatua ya kuangalia movie kamili kabisa na hasa kwa upande wa tablet ambazo ukubwa wa display ni kivutio katika multimedia.

8. Kupakua na kupakia
Hii ni sehemu yenye kuvutia mno, watu hupakua na kupakia mafaili kama vile ya muziki, video, picha na hata programu (apps) mbali mbali.

9. Kusoma habari
Kwa upande wa habari, hata watoa habari huchukulia tablet kuwa ni kifaa chenye kufaa zaidi. Magazeti mengi katika nchi zilizoendelea kama vile New York Times, The Times na The Sun tayari yanapatikana katika tablet na hata simu. Vile vile majarida makubwa kama Financial Times na The Economist hupatikana katika tablet mbali mbali na hasa iPad. Pia kuna majarida ya burudani, vichekesho na mafunzo mbali mbali. Mashirika ya habari makubwa yamekuwa wakiweka TV za live kwa njia ya streaming katika vifaa hivyo. Sky News, BBC na CNN zote zinapatikana kwenye tablet na simu.

 10. Kazi za Kiofisi
Kwa vile simu na tablet huja na Word processors, Spreadsheets, Database na presentation app, na vile vile kuna vifaa kama Blackberry vyenye usalama wa hali ya juu wengine wamekuwa wakifanya kazi za kiofisi katika vifaa hivi.

Ingawa haya si matumizi pekee ya vifaa hivi wengi hufanya mengi kati ya haya, lakini pia huu sio mwisho, uvumbuzi bado unaendelea, teknolojia kama GPS, acceletrometer, Gyroscope na digital compass tayari zimeshaleta matumizi mengi ya ziada katika vifaa hivi. Katika makala zijazo tunatarajia kuzungumzia matumizi ya simu katika siku za baadae.

Archos na Simu ya Ndani Yenye Android

 

Kampuni ya Ufaransa, Archos walitoa tablet muda mrefu kabla ya Apple kutoa iPad, ilikuwa ni tablet ya kwanza kutumia Windows 7. Kwa mara nyingine Archos imezitangulia kampuni nyingine kwa kutoa simu ya ndani (landline) inayotumia OS ya Android, hebu vuta fikra; unacheza Angry Birds kwenye simu ya ndani halafu unatumia skype, unasoma na kujibu email zako kisha unafanya video calling, hapo bado huna bili hata ya senti moja katika simu, ni intanet tu ndio inayofanya kazi. Simu hii inatumia protocol za DECT za kawaida na hivyo kuiwezesha kuunganisha kwenye line ya ADSL. La kuvutia zaidi katika simu hii ni kwamba Android market inapatikana, kwa hiyo una nafasi ya kuchagua apps zozote unazotaka kati ya laki tatu zilizopo kwenye soko hilo. Archos wameiita simu hii Archos 3.5 Smart Home Phone.

Jee huu utakuwa ni mwanzo wa ukiritimba wa Google katika simu za ndani? Tayari 48% ya simu za mkononi zinaendesha na OS ya Android inayotolewa na Google. Hii imezifanya simu zilizokataa kutumia OS hiyo ukiondoa  iPhone, kama vile Nokia karibu kusahauliwa katika soko la simu za hali ya juu, ingawa kwa sasa Windows Phone imetoa matumaini mapya kwa wale walioikataa Android.
Simu hii ina display yenye ukubwa wa 3.5” ikiwa na skrini ya kugusa. Huenda hii ikawa ni smartphone ya kwanza kuwa ni simu ya ndani. Inafanana kimaumbile na bidhaa nyingine za Archos na imetengenezwa na dock ambayo ndio yenye kuunganishwa na line ya simu, ukutani. Simu hii pia ina kamera yenye uwezo wa kurekodi video za HD katika kiwango cha 720p, ambapo maana yake ni kwamba unaweza kufanya high definition video calling. Archos hawakutoa tarehe ya kuanza mauzo ya simu hii wala bei yake, lakini inatarajiwa kuuzwa Faranga za Kifaransa nyingi tu ukilinganisha na simu nyingine za ndani. Kaa mkao wa kula mapinduzi katika simu za ndani yameanzia hapa.

Mtego wa Mbu, Eneo la Eka 1

 

Hebu fikiria ukinunua huu mtego sio tu utakuwa umejikinga wewe na watu wa nyumba yako na mbu bali huenda ukawa umeunusuru mtaa mzima na malaria, adha ya sauti za mbu  pamoja na vijipele vya kutafunwa nao. Dynatrap imetengenezwa maalum kwa ajili ya matumizi ya nje badala ya ndani ya nyumba kwa hiyo kwa wale wapanda milima, wakaa maskani, waweka kambi na kadhalika wao hasa ndio walengwa wa Dynatrap.  Hata hivyo kwa matumizi ya nyumbani inafaa kwa zile nyumba zilizozungushiwa uzio.  

Dynatrap ina taa aina ya florecent mbili ambazo huzalisha moinzi ya ultraviolet, mionzi hii hukutanishwa na gamba aina ya titanium dioxiding liliwekwa kwenye mtego huu na hivyo mchanganyiko huu huzalisha gesi aina ya carbon dioxide ambayo ndio hasa inayowavutia mbu na baadhi ya videde vingine vinavyoruka, harufu itokayo katika kijigajeti hichi ni sawa na ile ya binadamu anapopumua na kutoa gesi ya CO2 ambayo wadudu hawa ndio huvutika nayo.
Sasa ni vipi mbu au wadudu wengine hunaswa na mtego huu baada ya kuvutika na harufu hii? Dynatrap ina kijifeni fulani ambacho kina nguvu za kutosha cha kuwavuta wadudu wanapoikaribia, baada ya kuvutwa huingizwa kwenye neti ambapo hubaki humo mpaka wanapokufa. Ingawa kuna mitego mingi ya namna hii lakini kilichotuvutia kwenye mtego huu ni ule uwezo wa kuvutia wadudu katika eneo la mraba la eka nzima. Pia kivutio chengine ni kule kutokutumia kemikali zozote ambazo kwa kawaida hutoa athari fulani ama kwenye mazingira au binadamu mwenyewe. Bei ya mtego huu ndio tatizo, ni $199.95 za Marekani sio za Zimbabwe. Iwapo unataka kuuagiza mtego huu jina lake kamili ni One Acre Natural Attractant Mosquito Trap. Kama hizi fedha ni nyingi unaweza kujaribu kupigisha donation mtaani. Ni wazo tu.

Uchambuzi Wetu: BB Playbook V HTC Flyer

 

Mwaka 2011 ni mwaka wa tablet katika gajet. Tablet ambazo zimewachanganya watumiaji ambao wangependi ukubwa wa 7″ ni Blackberry playbook ya kampuni ya RIM iliyoko Kanada, na HTC Flyer iliyotolewa na kampuni ya Taiwan yaani HTC, zote tumezizungumzia katika makala zilizopita. Makala hii huenda ikasaidia kutoa jibu kwa wale ambao wana malengo ya kununua tablet hizi au kufahamu tu, kwani tutalinganisha, kuchambua ubora na kuangalia mustakbali wa miezi ya baadae wa tablet hizi juu ya nafasi ya kuboreshwa (upgrade) katika apps na OS. Huko nchini Marekani HTC Flyer inategemewa kutoka mwezi huu ikiwa na jina tofauti yaani HTC Evo View ambapo tofauti pekee ni kuwa Evo inakuja na teknolojia ya 4G. 


Vigezo vizuri: HTC Flyer

  • HTC Scribe ni uvumbuzi wa hali ya juu wa HTC ambao unaitofautisha tablet hii na nyingine zote.
  • HTC Sense mpya ambayo imetengezwa kwa mbwembwe za 3D katika mpishano, inatoa ladha mpya kabisa.
  • Widget mbali mbali zinarahisisha na kuboresha matumizi ya tablet hii.
Vigezo vizuri: Blackberry Playbook
  • Fremu kuwa ni sehemu ya kugusa (swipe) inatoa ladha ya aina yake katika matumizi ya tablet hii.
  • Blackberry OS Tablet aina ya QNX ni OS ya kipekee katika ulimwengu wa tablet.
  • Multitasking ni ya hali ya juu, kwa vile inaruhusu app isiyotumika (backbround) kuendelea kufanya kazi inaleta ufanisi.
Udhaifu: HTC Flyer
  • Imetumia Android Gingerbread 2.4 ambayo ni maalum kwa simu badala ya tablet.
Udhaifu: Blackberry Playbook
  • Apps ni chache mno kwa vile OS hii ni mpya (apps za simu za BB hazitumiki kwenye OS hii)
Ingawa Flyer imetoka mwanzo lakini Playbook ilitangazwa muda mrefu kabla ya Flyer, imewachukua RIM zaidi ya mwaka mmoja baina siku ya kutangazwa kwake na kutolewa kwa ajili ya mauzo, hii huenda ni kwa sababu RIM wameweka OS mpya ambayo bila shaka inachukua muda mrefu kuiandika na kuhakikisha kuwa haina bugs. Tuanze na vianisho halisi katika tablet hizi:

Matokeo ya awali: Sawa 5, HTC Flyer 4, Blackberry Playbook 7. Katika matokeo ya awali ni wazi kuwa RIM ni washindi, hata hivyo tunaingia raundi ya pili ili kupata mshindi wa jumla. Sasa tueleze na kuchambua ni kwa nini tumechagua mshindi kama tulivyochagua pamoja na mustakbali wa baadae wa tablet hizi na hivyo kujua mshindi wa jumla. 

Tukianza na mustakbali wa tableti hizi, HTC wana machache ya kufanya, kwanza huenda OS isiboreshwe kwenda kwenye Honeycomb  kwa vile Google hawaruhusu tablet zenye prosesa ya core moja kama ilivyo HTC Flyer kutumia Honeycomb, kwa hiyo kama kuna uboreshwaji maana yake HTC watalazimika kuwasubiri Google kutoa tolea linalofuata la Gingerbread. Kwa upande wa apps. Wakati HTC ni tegemezi wa Google, RIM kwa vile BB OS tablet ni yao wenyewe wana nafasi nzuri katika kuiendeleza OS hii kwa vile ni juhudi za kambi yao wenyewe ya OS. Hili tayari linaonekana kwa vile katika kipindi kisichozidi miezi mitatu RIM wameboresha OS yao mara mbili ambapo sasa imefikia tolea namba 1.0.6.2390, pia RIM wametangaza tolea kubwa la mabadiliko katika OS hiyo muda mchache ujao ambayo inategemewa kuingizwa apps kama vile email na BBM ambapo kwa sasa inategemea Blackberry Bridge (yaani kuunganisha tablet hii na simu ya BB) kwa maana hii kwa sasa watumiaji Playbook ambao hawatumii zimu za Blackberry wanakosa apps kadhaa muhimu ikijumuisha kalenda, BBM na Email.  Kwa hali mustabali wa baadae kwa upande wa OS ni kwamba RIM ni washindi pia.

Kwa upande wa bei, nchini Uingereza HTC Flyer inauzwa £579.00, tukilinganisha na Playbook yenye ukubwa sawa na HTC Flyer yaani 32GB, inauzwa £ 479.00. Ni wazi kuwa RIM pia ni washindi katika bei. Na huu ni ushindi mkubwa kwa vile £100.00 ambayo ndio tofauti unaweza kununua BB Curve mpya kwa ajili ya BB Bridge kwa kuongeza £19.00 tu, kulinganisha na bei ya HTC Flyer. 

Teknolojia ya Scribe ni ya aina yake, hapa ndipo ambapo kama mtu anataka kununua Flyer hii ni sababu tosha, kwa kifupi hii humuezesha mtumiaji kutumia kalamu maalum kuandika kwenye tablet hii na si stylus kama tulivyozoea, teknolojia hii hata hivyo ina udhaifu mmoja mkubwa, nao ni haitambui maandhishi (handwriting recognition) kwa hivyo ile dhana ya kuchukua tablet na kuandikia notes kwenye ukumbi wa mhadhara (lecture room) chuo kikuu au college bado haijatimia. Hata hivyo HTC walipoulizwa kama wanategemea kulifanya hilo hapo baadae walikataa kukubali au kukanusha, iwapo HTC wataliweza hili, basi HTC Flyer itakuwa ni chaguo la kwanza kwa wanafunzi na watu wa mikutano. 

Hata hivyo kwa wale wenye kasi ya kuandika kwa kibodi ya virtual kwenye skrini mguso, tayari HTC ni bora mno katika hili kwa vile ina uwezo wa kurekodi sauti wakati unaandika na baadae inakuruhusu kufanya marejeo ya maandishi na sauti kwa usambamba, yaani ukitaka kujua wakati unaandika paragrafu fulani mhadhiri au mwalimu alikuwa anasema nini, HTC Flyer ina uwezo wa kukufanyia hivyo kwa urahisi kabisa bila ya kwenda mbele na kurudi nyuma katika kutafuta ni nini kilisemwa wakati ule. Huu ni uvumbuzi wenye kurahisisha maisha wa HTC.

Mwisho kabisa tutaizungumzia Browser ya intanet. Browser tunaweza kusema ndio app muhimu na yenye kutumiwa zaidi kuliko apps zote. Kwa upande wa HTC zipo apps nyingi za Browser mbali ya ile inayokuja na Android, kwa mfano kuwa Opera Browser. Kwa upande wa Playbook inakuja na app yenye ufanisi bora zaidi katika matumizi, wakati zote zinakubali flash, multitasking katika Playbook ndiyo inayoifanya browser yake kuwa bora zaidi. Kwa mfano katika browser hii unaweza kudawnload file lolote hata wakati wewe unafanya kazi nyingine, file linaendelea kupakuliwa. 

Kiujumla ni kwamba sisi katika Gejetek tunaipa ushindi Blackberry Playbook kwa kwa sababu tatu za msingi, kwanza ina ubora wa mambo mengi kiujumla, pili mustakbali wake wa baada umo mikononi mwa RIM wenyewe ambao tayari wameonesha dhamira kubwa ya kuiboresha zaidi tablet hii na tatu ni Blackberry Bridge, yaani kutumia tablet hii kwa ushirikiano na simu ya Blackberry katika intanet na baadhi ya apps kumefanywa kwa ufanisi mzuri na wa hali ya juu kabisa. Pamoja na kuipa ushindi Playbook kwa sasa Flyer ina matumizi mengi zaidi kwa kule kuwepo kwa apps nyingi.

Amazon Kutoa Tablet

 

Amazon ni maarufu zaidi kwa kuuza vitabu, muziki, ebook reader na ebooks kwenye mtandao. Wauzaji hawa ebook reader aina ya Kindle iliyopata umaarufu mkubwa inasemekana kwamba wako njiani kutoa kompyuta aina tablet. Hii bila ya shaka inazidi kuweka mashakani mustakbali wa ebook reader ambapo tangu kuingia kwa tablet wanunuzi wengi wamekuwa wakipendelea zaidi kununua tablet kuliko ebook reader, ingawa Amazon hawakuthibitisha moja kwa moja juu ya hili, pale Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hii Jeff Bezos alipozungumza na wadau wa  Consumer Reports alipohojiwa kuhusu tablet hiyo alichosema ni ‘stay tuned’, akiwa na maana utafika wakati wa kukujulisheni juu ya hili. 
Ingawa Amazon hawakuzungumzia chochote juu ya tablet hiyo, wadau katika fani ya tablet wanadhani kuwa tablet hii haitakuwa ni ya hali ya juu, italenga zaidi kuendeleza biashara za Amazon ambazo ni Muziki, vitabu vya elekroniki (ebooks), na michezo ya sinema (movies). Amazon pia wanatarajiwa kuruhusu watumiaji wa tablet hiyo kuangalia video bure ukiwa mtandaoni (Streaming) ikiwa ni sehemu ya utangazaji (promotion) wa tablet hii.
Tablet hii inategemewa kutoa ushindani zaidi na iPad kwa vile tayari Amazon wana nyimbo, video na vitabu kwa kutosha kutoa upinzani kwa Appstore, kwa upande wa Apps kwa vile tablet hii itatumia OS ya Android haitakuwa ni tatizo kubwa ingawa, Android 3.0 Honeycomb inakabiliwa na ukame wa Apps kwani Apps zaidi ya laki tatu zilizo kwenye Android Market ni kwa ajili ya Android 2.4 kwenda nyuma ambazo ni za simu tu. 
Pamoja na uhaba wa apps katika honeycomb, uongezekaji wa apps mpya katika platfomu hiyo ni wa kasi ya hali ya juu tofauti na platfomu nyingine kama vile za Blackberry Playbook na HP (Web OS) ambao wanaonekana wazi kuwa ni wenye kuwa na kasi isiyoridhisha.
Tukizingatia kwamba tablet ni kwa ajili ya kazi tano muhimu, nazo ni mawasiliano na hasa email, kutumia mtandao, multimedia (muziki, picha na video), games na kusoma vitabu vya elektroniki, Amazon watakuwa ni kampuni sahihi kabisa kutoa tablet, kwa vile yote tuliyoyaelezea tayari Amazon ni wenye kuwa nayo. Mbali na hayo Amazon pia ina mpango wa kuuza  apps zao wenyewe. 

Nokia N9 yatinga na Meego OS

Mbali na kutangaza wazi kuwa wanajiunga na Windows Phone 7 sasa Nokia wamekuja na kifaa sio cha kawaida kikiwa kinatumia OS ya MeeGo. Hii inadhihirisha wazi dhamira ya Nokia kuachana kabisa na Symbian OS. Nokia wamechelewa mno katika uamuzi huu, kampuni zote nyingine ikiwa ni pamoja na Samsung, Life is Good (LG) na Sony Ericsson wameachana na OS ya Symbian kwa muda mrefu sasa. Hata hivyo kutumia kwao MeeGo OS pia kunaonyesha ni wazi kuwa Nokia walikuwa na dhamira ya kupambana na Android ya Google. MeeGo na Android ni OS zenye asili ya Linux, OS  ya MeeGo inaendelezwa kwa ushirikiano wa Nokia na Intel baada ya kampuni hizo kuunganisha juhudi zao za zamani katika OS ambazo ni Moblin ya Intel na Maemo ya Nokia. Simu hii itajulikana kama Nokia N9. Hata hivyo MeeGo OS bado ni changa kwani imetangazwa mwaka 2010. Nokia N9 itakuwa ni simu ya kwanza kutumia MeeGo OS lakini pia huenda ikawa ni ya mwisho kwa ule maktaba wa Nokia kutumia Windows Phone 7

Umbile la Nokia N9 ni lenye kuvutia mno machoni, umbile ambalo tunaweza kuliita jipya kwani hakuna simu inayofanana na Nokia hiyo. La kwanza kabisa ni kwamba simu hiyo haina hata kifungo (button) kimoja mbele. Vianisho halisi vya simu hiyo ni vya hali ya juu, ni wazi kwamba Nokia wamekuja na hasira wakitaka kurudi mchezoni na kutambulika kama zamani. Vianisho halisi hivyo: 
RAM: Gigabyte moja, hii inaonekana kama ni jambo la kawaida kwa sasa kwani simu zote  ambazo ni za kiwango cha juu zina RAM hii. Hata hivyo gigabyte moja inatosha kabisa kuifanya simu kufanya kazi kwa ufanisi. 
Diplay: ina ukubwa wa 3.9” ikiwa na mvimbo wa aina fulani (Concave), imeizidi iPhone 4 kwa 0.4”, ni muhimu kufahamu kuwa simu zote ambazo huwa katika simu bora zina display yenye ukubwa kati ya 3.5” na 4.3”
Prosesa: Ina kasi ya gigabyte nzima, sawa na ile iliyotumika kwenye Samsung Galaxy S2 ambayo wengi wanaiona kama ni simu bora kwa sasa. 
Hard Drive: Simu hiyo pia ina drive aina solid state (SSD) yenye ukubwa kuanzia gigabyte 16 hadi 64, iPhone imeishia 32GB na hivyo hii inaifanya Nokia hii kuwa ni simu yenye drive ya ndani kubwa zaidi kuliko simu zote.
Kamera: ina megapikseli 8 pamoja na lenzi aina ya Karl Seiss ambayo hutumika sana kwenye kamera aina ya Sony. Kamera hiyo pia ina flashi na uwezo wa kurekodi video za HD katika kiwango cha 1080p kamili. 
Ikiwa hujatosheka na ubora wa hali ya juu wa vianisho hivi simu hii pia itakuwa ni ya kwanza kuwa na teknolojia ya Dolby Digital Plus pamoja na Dolby headphones post prosessing ambayo itakufanya usikie sauti safi na kali aina ya surround. Pia simu hiyo itatumia Micro Sim kama zile zilizotumika kwenye iPhone 4 na iPad zote zenye 3G. Nokia N9 pia ina Near Field Technology (NFC) ambayo itaiwezesha simu hiyo kusoma habari mbali mbali za digital kama vile kulipa supermarket baada ya simu hiyo kuingizwa tarakimu zote zinazohusiana na akaunti yako ya fedha. Simu hii pia ina GPS.
Simu hiyo itakapotolewa itakuwa tayari ina baadhi ya games ambazo ni maarufu ikiwa ni pamoja na Angry Birds, Galaxy on Fire 2 na Real Golf 2011.  Sisi katika Gajetek tunadhani kuwa simu hii itakapotolewa itakuwa na nafasi nzuri ya kukaa kwenye simu kumi bora Duniani, angalau kwa muda mchache, hii pia itategemea na simu nyingine mpya zitakuwa vipi. Pia bila ya shaka yoyote OS ya MeeGo italeta mapinduzi mapya katika simu za mkononi. Kasoro kubwa katika OS hii itakuwa ni uchache wa apps kama ilivyo kwenye OS yoyote mpya. Hata hivyo kuna uvumi kwamba katika makubaliano ya Nokia na Microsoft kujiunga na kambi ya Windows Phone, Nokia watalazimika kuacha kuiendeleza MeeGo OS, ikiwa hili ni kweli hizi ni habari za kusikitisha, kwani wateja ni bora kwao kuwe na nafasi ya kuchagua baina ya OS mbali mbali na hivyo kuondoa uwezekano wa ukiritimba katika soko. Hata hivyo ni kwa nini Nokia watumie OS ambayo ni miezi michache ijayo inabidi kuachana nayo? Haya ni mambo ya kushangaza kwa upande wa mikakati ya Nokia, kampuni ambayo imepoteza hisa kubwa katika mauzo ya simu Duniani baada ya kuingia kwa Android na iPhone, takriban miaka mitano iliyopita. 

Laptop a Mionzi ya Jua Madukani

 

Hivi karibuni tulizungumzia laptop iliyotolewa na Fujitsu ambayo itatumia nguvu za jua, katika muda usiozidi mwezi Samsung wametangaza kuwa wanatarajia kuiingiza laptop kama hiyo madukani, nayo ni Samsung NC215S, iko tayari kwa mauzo, itatolewa huko Urusi mwezi wa nane na kisha kuuzwa huko Marekani. Hii ni netbook zaidi kuliko laptop kwani ina display yenye ukubwa wa 10.1” tu.

Vianisho halisi vingine ni pamoja na RAM GB moja na prosesa aina ya Atom yenye core moja tu. Kwa upande wa Hard Drive Samsung wamewapa nafasi wateja kuchagua moja kati ya aina mbili nazo ni 250GB na 320GB.

 Kivutio zaidi cha laptop hii ni kule kujichaji kwa kutumia mionzi ya jua, hili pia linakwenda sambamba na skrini ambayo inaweza kutumika juani. Samsung wameweka kwenye dislay ya kompyuta hii teknolojia maalum itakayoruhusu matumizi hayo, dislay hii ambayo ina rezolushani  1024 x 600 pia ina mwangaza  wa kiasi cha 300cd/m2 na uwezo wa kutoakisi mwangaza wa jua na hivyo kufanya kuitumia ukiwa umekaa juani sio tatizo kama zilivyo laptop nyingi nyingine. Chaji kamili katika netbook hii itakuwezesha kuitumia kwa muda wa masaa kumi na nne na nusu. Netbook hii itauzwa huko Marekani kwa $400.00 na nchini Urusi itauzwa $500.00, hatufahamu ni kwa nini bei zimetofautiana kiasi hiki lakini huenda ikawa ni mambo uya kodi au huenda kwa sababu huko Urusi umeme bado unakatika katika.

Microsoft Kushirikiana Na Wachakachuaji

 

Kampuni ya Microsoft katika hali isiyo ya kawaida imeamua kushirikiana na wachakachuaji wa Windows Phone 7 na  kuwafanya Sony na Apple kuonekana kama kwamba si wenye busara. Makundi ya Jailbreakers au hackers wa Windows Phone wanaojiita ChevronWP7 na Redmond wameruhusiwa rasmi na Microsoft kuingiza apps na mambo mengine ambayo awali yalikuwa yakitumika kupitia mlango nyuma tu katika Windows Phone 7, walifanya hivyo kwa vile walikuwa hawatambuliwi rasmi na Microsoft. Makundi haya yanapenda zaidi kutambulika kama Homebrew Communities (Jamii za watengeneza apps na waendelezaji wa OS binafsi) kuliko hackers. Homebrew Communities hubadili firmware (OS), hutengeza apps na kufungua (unlocking) gajeti hizo. Pia huwa na tabia za kutumia API ambazo haziruhusiwi na hivyo kuwapa nafasi kufanya mambo ambayo developers watiifu hawawezi kuyafanya.
Apple katika vifaa vya iOS yaani iPad, iPod Touch, iPhone na Apple TV wamekuwa wakicheza mchezo kufukuzana wa paka na panya na Makundi haya ya homebrew developers au jailbrekers, baada ya Apple kushindwa mahakamani kufanya kuwa jailbreaking ni kinyume cha sheria. Makundi mbali mbali ya hackers na developers kupitia Cydia na masoko mengine yamekuwa yakijailbreak gajeti hizo na kuingiza apps zao wenyewe. Hata hivyo kila pale ambapo Apple wamekuwa wakiboresha Firmware zao (OS) wamekuwa wakizifunga tena gajeti hizo na hivyo kuwafanya wachakachuaji hao kutafuta njia nyingine ya ku-jailbreak. Mchezo huu pia umekuwa ukiendelea baina ya hackers na kampuni ya Sony katika Playstation 3 na PSP.
Hatua hii inaelekea kwamba Microsoft wamekubaliana na hackers hawa kwa lengo la kuua uuzaji na ugawaji bure wa apps kwa makundi hayo, kwani baada ya makubaliano haya kwa sasa Apps za Redmond na ChevronWP7 zitakuwa zinauzwa. Hivyo Microsoft wataweza kupata hisa fulani katika mapato ya hackers hawa. Hii ni njiia ya busara zadi ya vita dhidi ya hackers badala ya kujaribu kutowatambua na kushindana nao jambo ambalo si Apple au Sony wala hackers wanaonekana kupata ushindi.


Wakati kwa upande wa Microsoft huu unaelekea kuwa ni ushindi mkubwa dhidi ya wachakachuaji, kwa upande wa wachakachuaji huu unaonekana kuwa ni usaliti dhidi yao  kwani muda si mrefu Chevron na Redmond watalazimika kuwa watiifu kwa Microsoft, hivyo hawatatofautiana na developers wa kawaida. Lakini je wachakachuaji wote watakuabaliana na Microsoft? Ni muda tu ndio utakaojibu suali hili, lakini pia tukumbuke kwamba pesa inaweza kumtoa raisi ikulu.

Faida kubwa inayopatikana kwa watumiaji wa kawaida katika Jailbreaking ni kupata apps, themes na vitu kama hivi ambayo huwezi kuvipata kwenye Appstore ya Apple na kwa upande wa Playstation humuwezesha mtumiaji kuingiza DVD za game ambazo ni copy. Hasara kubwa ni kuwa kila mara inakubidi kujailbreak upya kifaa chako na pia mara nyingi vifaa venye kuwanyiwa jailbreak hupoteza uimara au utulivu (stability) wa OS. Na kwa upande wa Sony imekuwa ikiwafungia kucheza online wale wote wenye kuchakachua kwenye Playstation zao.

Mercedes Benz Dhana ya 2013

 

Kama kuna gari ambayo imeifanya Mercedes Benz ionekane ni gari ya kawaida tu ni Mercedes Benz A Class, Mercedes walilenga soko la gari za bei nafuu, gari hii inauzwa kuanzia £16,000.00 (TSh 41,142,488.00) ukilinganisha na Benz kama vile GL500 ambayo itakubidi utoe  £72,000.00 (TSh 185,141,200.00) kama unataka kuendesha tangu ikiwa mpya, utaona kwamba kuna tofauti kati ya gari hizi ya zaidi ya Shilingi Milioni 143. Sasa tofauti haiko katika bei tu bali hata katika gari zenyewe. Gari hii ilitoka nje ya mstari ambao Benz wameuchora miaka mingi na hivyo kufahamika na watu kama ni gari ya kifakhari.

Mercedes wameliona hili na sasa wametoa gari dhana (Concept Car) ambayo itaanza kuuzwa mwaka 2013 aina ya A Class ambayo sio tu itairudishia hadhi Mercedes bali pia inatoa mawazo na picha ni vipi gari za miaka michache ijayo zitakuwa tofauti kabisa na gari tunazoendesha leo.  A Class concept imetimia, gajeti ya kujiburidishia ni iPad, bila ya shaka kwa wakati zinaingia katika soko itakuwa ni iPad 4, hata Steve Jobs mwenyewe hajui itakuwa vipi, kwani kwa sasa Apple wanaifanyia kazi iPad 3.
Maumbile ya gari hii ni kama kwamba imetoka sayari nyingine, ina milango mitatu aina ya coupe, inataka kufanana na Vauxhall Astra, lakini inaifanya astra ya 2010 ionekane kama gari ya miaka 10 nyuma. Gari hii itakuwa na kipaa cha kioo kitupu, dashi bodi ya gari hii imetengenezwa kwa kuiga umbile la bawa la ndege (ndege ya abiria)  ambapo dashi hii ni yenye kuonesha ndani (transclusent), pia undege katika gari hii unaonekana kwenye sehemu za kuingizia hewa (vent) ambazo zimetangezwa kama injini ya ndege inayoning’inia kwenye mabawa yake. 
Gari hii ambayo ni wazi imelenga kutoa upinzani kwa BMW 1 Series na Audi A3 itakuwa ni bora zaidi kuliko wapinzani wake, ingawa ni matarajio yetu kwamba ifikapo 2013 Audi na BMW nao wataboresha gari zao katika matoleo yajayo. Gari hii kwa upande wa teknolojia itakiwa ni ya aina yake. Taa zake ni aina ya LED zenye umbile la ubawa wa ndege na nguvu za hali ya juu. Ina uwezo wa kusimama wenyewe pale ambapo kutatokea hatari na dereva kuchelewa kupiga breki, itakuwa inampasha dereva juu ya habari mbali mbali anazozihitaji akiwa anaendesha kama vile kasi inayoruhusiwa katika barabara, taa nyekundu na kadhalika.
Skrini ya dashi itakuwa inatoa taswira za 3D katika rangi mbali mbali hata hivyo magenta ndio itakayotawala, pia gari hii itakuwa na kile ambacho Mercedes wamekiita Command online ambapo itamuwezesha dereva kutumia gajeti za mawasiliano kama vile simu kwa usalama huku gajeti hizi zikiwa na uwezo wa kuingia kwenye mtandao kupitia kampuni ya Mercedes.
Kuhusu injini gari hii itabeba sawa na ile iliyoko kwenye M Class 270, ukizingatia kwamba A Class dhana ni Coupe bila ya shaka gari hii itakuwa na nguvu za ajabu. Injini hiyo ambayo itakuwa ni ya Petroli badala ya umeme (betri) kama tulivyozoea kuona kwenye gari mpya, itakuwa si yenye uchafuzi mkubwa wa mazingira ingawa Mercedes hawakutoa takwimu kamili za utoaji wa moshi mchafu (carbon emmission).
Gari hii itakuwa inabeba abiria watatu pamoja na dereva, itakuwa na viti ambavyo vinafanana na vile vya gari za Formula 1. Mercedes hawakutangaza bei ya gari hii ingawa wengi wanatarajia kuwa haitafanana na zile A Class zilizoitangulia bali itakuwa ni ya bei ya juu zaidi.

Uchambuzi Wetu: iOS 5 Baada ya Kuitumia

 

iOS 5 ikitoa nafasi kwa anaetaka kununua nafasi zaidi katika iCloud
iOS 5 imekuja na mambo mapya karibu 200, Steve Jobs na wenziwe katika uzinduzi wao alizungumzia mambo kumi tu mapya. Gajetek tumeitia mkononi iOS 5 beta katika iPad 2 na iPhone 4, na sasa tunakuchambulieni mambo machache ambayo tunadhani ni muhimu kuyafahamu. Tuanze na iCouds, wakati Apple imetangaza kuwa huduma hii ni bure wengi walipata nafuu, lakini wale waliozoea MobileMe na watu wenye matumizi makubwa walisikitishwa na ‘storage’ ndogo ambayo Apple wametoa yaani 5GB tu, katika kuipekua pekua tumekuta kwamba watumiaji ambao hawatatosheka na 5GB wataweza kununua nafasi zaidi, huduma hii haitegemewi kuanza wakati huu wa majaribio mpaka pale iOS 5 kamili itakapotolewa kwa wote. Hata hivyo katika wakati huu wa majaribio iCloud haikukamilika katika ufanyaji wake kazi kama ilivyoelezewa katika WWDC, lakini pia ina mambo ya kutosha ya kukufanya uhisi mabadiliko.

iMessage kwa sasa imechanganywa na Message (yaani text message) hatuna uhakika kama Apple wataitenganisha baada ya toleo la majaribio (beta) au itabaki hivyo hivyo. Lakini tumevutiwa na ubinafsishaji (customisation) ambao unaweza kuufanya katika chat za iMessage kama vile kuruhusu aliyekutumia ujumbe ajulishwe ama asijulishwe kama ujumbe umeusoma, kurudia kuzinduliwa kwa mtumiaji iwapo amepata iMessage na mengi mengine.
Notification Center ya iOS 5
Notification Center pia imetuvutia kiasi fulani ingawa ni wazi inaonekana kwamba huu ni wizi wa mawazo kutoka Android ya Google, unaposugua (swipe) simu, iPod Touch au iPad kutoka juu kuja chini,  inashuka skrini ya Notification ambayo itakuonesha vitu kama vile facebook update, twitter, message na imessage mpya, misscall na reminders ambazo bado hujaziangalia. Notification center inaleta ufanisi mkubwa katika iOS kwa vile inarahisisha kuepuka kupitia kila app kujua nini kinajiri katika app ile hasa ukizingatia utaratibu wa app za iPhone, iPad na iPod Touch kuwa ni icons tu ambazo haziko active au live kama zile za Android ambazo zina ‘active widgets’ na Playbook ambayo ina ‘live multitasking’. Hata hivyo app ya notification center haipo bado kwa hiyo mambo yote yapo kwenye settings. Tunadhani kwamba itabaki kuwa hivyo hata baada ya kutolewa toleo la mwisho la iOS 5.
Huduma ya Facetime kwa sasa imeboreshwa ikiwa ni pamoja na kuruhusu kupigiwa simu hii ya video kupitia email zaidi ya moja katika kifaa kimoja mbali na ile Apple ID au namba ya simu kama ilivyokuwa zamani. 
App ya Newstand bado haikuanza kufanya kazi unapopakua magazeti na majarida kutoka app store bado yanabaki kuwa kama app zilizo pekee (stand alone apps) badala ya kuwekwa pamoja katika app hii, hii inategemewa kuanza kazi katika beta ya pili ambayo itatoka kabla ya iOS 5 kamili kutolewa. Kwa upande wa twitter, inaonekana tayari imeanza kufanya kazi ikiwa kama sehemu ya iOS kwa vile imo katika notification center iwapo uta login kwenye settings na app badala ya app peke yake.
Wakati hapo awali Apple walikuwa hawaruhusu kutumia email ya MobileMe kama Apple ID yako sasa ni kinyume, unaweza kutumia email zao yaani jinalako@me.com  au jinalako@mac.com kama Apple ID. Hii ni kutokana na kwamba email hizi sasa si ya kulipia tena bali ni bure. Hapo awali walihofia kwamba iwapo hujalipia huduma ya MobileMe na kufungiwa, akaunti zako za iOS Appstore na Mac AppStore zingekuwa matatani. 
Wakati sync ya iTunes bila ya waya haijaanza, sync ya iClouds tayari inafanya kazi, hata hivyo Apple inabidi watafute njia ya baaadhi ya matatizo yaliyojitokeza ikiwa ni pamoja na ku-syinc apps na vitabu ambavyo wewe umevifuta, huwa haichagui inaangalia apps zote ambazo umenunua na kuzidownload, huchelewi kujikuta una apps zaidi ya 400 ikiwa ni pamoja na zile ambazo ulitaka kuzijaribu tu kwa vile zilikuwa bure.
Safari, kamera na picha tayari zina sync kwenye iCloud na pia safari ina tab nyingi kama ilivyoelezewa, picha ambazo zinakaa kwenye iPad, iPod Touch na iPhone ni 1000 kutoka kwenye iCloud na kompyuta haina kiwango maalum, hata 1,000,000 itahifadhi ushindwe wewe au disk ya kompyuta yako.
Kwa wale ambao wangependa kuijaribu iOS hii kwa sasa inapatikana kwa developers na watundu watundu wenye kujua mambo ya kuchakachua, unaweza kutuandikia kwenye gajetek@gejetek.com kwa ushauri zaidi juu ya hili, tungeomba watumiaji ambao sio watundu wa kompyuta wasijaribu hili, huenda likawaletea taabu, ni vyema tu usubiri mwezi wa Septemba itakapotoka iOS 5 kamili. Tutachambua tena pale Apple watakapotoa Beta ya pili ya iOS 5.

RIM na Blackberry Zao Taabani!

 

Kampuni ya RIM inaonekana kuchechemea mno katika mauzo baada ya kutoa ripoti ya nusu mwaka, habari hizi hazitawapendeza watumiaji wa BBM na zitawatia mashaka wawekezaji katika RIM, kwa vile hili linaiweka kampuni hii katika utata kwa miaka ijayo. Pamoja na RIM kutoa tablet mpya haikusaidia kuinua mauzo ya kampuni hiyo kwani mpaka sasa RIM wameuza Playbook 500,000 tu. 
Sababu mbali mbali zimetolewa kutokana na hali hii ambayo inaikabili RIM,  zikiwezo za nje ya kampuni na za ndani pia. Wakati RIM kama Facebook inaonekana kuendelea kustawi katika nchi zinazoendelea, katika nchi za Dunia ya kwanza kampuni hizi zimeonekana kutoa dalili kwamba karibu zinagonga mwamba. Bado CEO mtoto (Toddler CEO) Mark Zuckerburg wa Facebook hana haja ya kuanza kukosa usingizi, Afisa Mtendaji Mkuu Mwenza (Co-CEO) wa RIM Bw. Mike Lazaridiz ambaye ndiye mwanzilishi wa kampuni hii, inawezekana kabisa kuwa usingizi kwake sasa ni kitu ghali mno.

Takwimu zifuatazo zinathibitisha hilo kwamba kampuni hiyo iliyopo Kanada kuwa pamoja na kwamba haikupata hasara lakini haikufikia malengo na matarajio yaliyowekwa: 
1. Mapato yaliyotangazwa baada ya kufungwa kwa soko la hisa (Wall Street) kuwa ni $4.9 milioni, baada ya kuzingatia ugumu na ushindani wa kibiashara na hivyo kupunguza kiwango wachambuzi na watabiri wa mambo ya soko la hisa walitarajia RIM iwe na mapato yasiyopungua $5.2 Milioni. 
2. Pato hili lina maana ya kushuka kwa mapato ya RIM kwa 12% kulinganisha na kipindi kama hichi mwaka jana. 
3. Kutokana na kupotea kwa kujiamini kwa wawekezaji, hisa za kampuni hiyo imeshuka thamani kwa 10%. 
Ni wazi kwamba RIM wanakoelekea ni tishio kwa kampuni hiyo, lakini RIM wamekiri kuwepo kwa matatizo na hivyo wamechukua hatua mbili muhimu ili kuiweka kampuni hii katika hali ya ustawi. Kwanza ili kuwarudishia wawekezaji katika kampuni hii RIM imenunua hisa ili kuwarudishia wawekezaji uaminifu huo. Pili RIM ambayo ina wafanyakazi 17,500 tayari imetangaza kupunguza wafanyakazi katika kampuni yao. 
Sasa tuingie kwenye uchambuzi wetu ni nini hasa kilichopelekea kuanza kuanguka kwa watengenezaji wa Blackberry. Tukianza na sababu za nje. Apple na Google wana mchango mkubwa wa kuanguka kwa RIM na Blackberry zao. Sasa hivi. IPhone na simu za Android zimekuwa hisa kubwa ya mauzo ya simu na hivyo kupelekea kuanguka kwa Blackberry. 
Tukija na sababu za ndani ya RIM, Blackberry zina udhaifu katika vifaa (hardware) vile vile na Programu (Software) ukilinganisha na iPhone pamoja na simu kama vile za HTC, Samsung, Motorola na LG ambazo zinatumia Android. Hivyo hii inapelekea kuanguka kwa Blackberry. Kwa sasa Blackberyy inaonekana kuwa ni simu ya vijana au watumiaji wa BBM. Katika ulimwengu wa ‘Smartphone’ ambapo simu imekuwa na uwezo sawa na kompyuta kwa utendaji lakini ndogo kwa umbile tu, hutegemei kuwa utabaki kwenye ushindani kwa kutegemea BBM tu.
RIM wanafanya biashara wakionekana kama kwamba hawana haraka. Kwa mfano imewachukua zaidi ya miezi mitano kuanza mauzo ya Playbook Ulaya kwa zaidi ya miezi minne baada ya kutolewa huko Marekani. Matokeo yake baada ya miezi yote hiyo ni RIM wameuza Playbook 500,000 tu. Ni nini hasa kinachowachelewesha? 
RIM hawana budi kubadili OS yao, kwani BB OS 6 bado haitoi ushindani, inachosikisha na kuenesha wazi kwamba RIM bado hawajapata somo, BB OS 7 siyo ya QNX, ile iliyotumika kwenye BB Playbook. Wengi wamevutiwa na OS hii mpya na matarajio yalikuwa kwamba OS7 ya Simu yatatumia OS kama hiyo. 
Iwapo RIM wanataka kubaki mchezoni ni lazima waboreshe vifaa vyao na OS zao ziendane na wakati viweze kuvutia developers (watengeneza apps) na wanunuzi wa simu. Iwapo watachelewa huenda baada ya miaka michache tu tukatembelea makaburi ya RIM na Blackberry. RIM lazima wajue kwamba maji hujaa na kukupwa kwa wakati.

Blogi ya habari huru zisizo na upendeleo na uchambuzi yakinifu kuhusu Gajeti na Teknolojia Duniani