Uchambuzi Wetu: Matumizi ya Simu Miaka ya Baadae

 

Simu ni kifaa kilichopata mabadiliko ya haraka, ningali naikumbuka Nokia Ringo na Motorola Startec, simu za mwanzoni kabisa kuingia Tanzania wakati wa enzi za Mobitel. Ukifananisha simu zile na hata simu ambayo leo tunaiona kuwa ni kimeo, basi utakubali kuwa simu ni kifaa kilichobadilika mno na tena kwa haraka sana. Katika makala hii tunajaribu kuangalia mbele, ni vipi tutaitumia simu katika maisha yetu hapo baadae. Ni vigumu kuwa sahihi kwa asilimia mia moja, lakini tunaamini haya tutakayoyaelezea yatatokea. Kutokana na teknolojia mbali mbali kuingizwa kwenye simu, teknolojia kama vile Gyroscope, Near Field Communication (NFC), GPS, Digital Compass, Accelerometer na sensa nyingine mbali mbali simu itakuwa ni kifaa chenye matumizi ya ajabu kabisa, mbali na kuwa itatumika kiajabu. Yafutayo ni baadhi tu ya mambo ambayo simu itakuwa inauwezo wa kuyafanya miaka michache ijayo, yaani tunazungumzia chini ya miaka kumi hivi.

Simu kama pesa: itachukua nafasi ya kadi za benki, teknolojia ya NFC inaipa nafasi kubwa sana simu kufanya hili, tayari teknolojia hii imeshaanza kutumika, kwa mfano kampuni ya Orange hukubali malipo ya chini ya £15.00 nchini Uingereza kwa kutmia simu zao, ambazo zimeingizwa taarifa za kadi yako ya benki. Nchini Marekani Google wameanzisha huduma waliyoiita Google Wallet, ambayo nayo inakuwezesha kufanya mali[po kwa kutumia simu.
Kitambulisho: Simu kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi data, inaweza kuwa ni kitambulisho chako, kwa vile inauwezo wa kuhifadhi finger print au taarifa nyingine zozote za ‘artificial intellingence’. Kwa hiyo simu inaweza kuwa leseni au hata pasipoti. Sitoshaangaa baada ya miaka kadha mtu asafiri na simu badala ya pasipoti na ticket.
Funguo za Gari: Tayari BMW na kampuni nyingine wameshatoa gari ambayo inafunguliwa kwa Fob, teknolojia hii inaweza kuingizwa kwenye simu, tayari kuna gari ambazo zinawashwa na iPhone 4, kama vile BMW x5 zilizotoka kuania mwaka 2010. 
Funguo za Milango: Teknolojia ya Fob inaweza na tayari inatumika kufungulia milango kwa hiyo hili nalo linawezekana na si mud amrefu watu watafungual milango ya nyumbani au kazini kwa kutumia simu zao.
Box la TV: Simu tayari ina uwezo wa kuwa mbadala ya DVD, muda si mferu itakuwa ni mbadala wa box la TV (Set top Box), tayari HTC Flyer ikitumia huduma ya streaming wanakodisha movies kwenye tablet hii, bila ya shaka huduma hii itakuwepo kwenye simu za HTC zijazo, nchini Uingereza  Skysports wanaonyesha mechi za La Liga na Primier League kwenye iPhone kwa gharama za £8.00 kwa mwezi. Ninazungumzia mechi kama zinavyojiri (live stremaing), weka na huduma ya iCloud bial ya shaka huko mbele mambo yatakuwa moto.
Game Console: tutakuwa hatuhitaji PS3 wala PS10, ni simu tu. Mwezi wa tisa Real Race itakuwa ni game ya kwanza kutoka kwenye iPhone kwa msaada wa Apple TV itaonesha kwenye TV moja kwa moja na hivyo iPhone itakuwa ni kontrola tu.
Simu kama Daktari: Tayari iPhone inaweza kutumika kama kifaa cha kupimia BP, muda si mrefu simu zitakuwa ni kama kifaa cha kidaktari kufanya mambo kama kuchukua vipimo kwa joto la mwili, BP, sukari ya mwili na vipimo viengine. Vile vile Chuo Kiku cha Carlifnia tayari kimo mbioni kutengeneza kifaa cha kupimia Malaria kitakachotumika kwenye simu.

Kamera na Kamkoda: Ingawa kwa sasa simu zina kamera na kamkoda bado watu wanaendelea kuona umuhimu wa kuwa na vifaa hivyo kwa vile tu teknolijia hizi bado zimo njiani kuboreka kuelekea kwenye kiwango cha kitaalam au cha hali ya juu kinachopatikana kwenye gajeti hizi. Si muda mrefu hatutahitaji tena kuwa na kamkoda au kamera kama vifaa pekee bali simu itatosheleza mahitaji haya, kwa upande wa kamera watu wenye simu kama vile iPhone 4, Samsung Galaxy S 2 na HTC Evo 3D hawaoni tena umuhimu wa kuwa na kamera.

Kwenye makala zijato tutajaribu kuangalia simu za baadae zitakuwa vipi kimaumbile na kutumiaka namna gani, kwa sasa ni kibodi, skrini za kugusa, amri za sauti (voice command) na kadhalika. Ni vipi simu zatatumika baadae? Endelea kutembelea tovuti hii.
Advertisements

Uchambuzi Wetu: Blackberry Bridge

 

Research In Motion, watengenezaji wa simu za blackberry bado hawako nyuma katika uvumbuzi na uboreshaji wa bidhaa zao mbali mbali. Mwaka huu RIM wametoa tablet yao ya kwanza, Blackberry Playbook, katika tablet hii wamekuja na kile walichokiita Blackberry Bridge, huduma hii inaunganisha simu yoyote ya Blackberry inayotumia Blackberry OS toleo la 4 kwenda mbele na BB Playbook, unapounganisha tablet na simu ya Blackberry kwa njia ya Bluetooth na kupitia app ya BB Bridge unapata faida za kutumia internet ya simu yako kwenye Playbook kupitia Bridge Browser (tethering), pia inakuruhusu kutumia apps za Messeges, Contacts, Calender, BBM, Memopad, Tasks na Bridge Files.
Uchambuzi Wetu utajaribu kuangalia manufaa na hasara ya huduma hii ya kipekee waliokuja nayo RIM katika Blackberry Playbook. Kabla hatujaingia katika uchambuzi ni muhimu tufahamu kwamba ikondoa Browser, apps zote nyingine ambazo zimo kwenye Bridge hazipatikani kwenye Playbook bila kufanya bridge. ukiangalia umuhimu wa apps hizo, hii ina maana kwamba Playbook inakaribia kuwa haina maana bila ya kuwa na simu ya Blackberry. Tukianza na uchambuzi, bila ya shaka RIM wamefanya hivi ili kuwalazimishsa watakaonunua Playbook kununua pia simu ya Blackberry. Kwa hiyo kama wewe ni mtumiaji wa simu za Android, iPhone au Windows Phone, fikiria mara mbili kabla ya kununua Blackberry Playbook.
Wakati Playbook haitumii 3G au 4G kwa sasa, kwa maana ya kwamba haiingii kadi ya sim, lilikuwa ni wazo sahihi kabisa kuweka Bridge Browser ili kunufaika na internet ya simu pale ambapo uko pahala usipoweza kupata WiFi. Hapa RIM wamecheza kama Pele. Ni ugunduzi mzuri tena wenye manufaa kwa kiasi kikubwa, kwa vile tumefika mahala ambapo tunajiuliza tutakuwa na gajeti zenye kadi za sim ngapi, simu inatumia kadi hiyo, ongeza tablet, ongeza na game (PS Vita  pia itakuwa na sim) na hivyo kuwa na bili chungu nzima. Kwa hiyo RIM wametuepushia kulipia internet za 3G mara zaidi ya moja baina ya tablet na simu.
Wakati Bridge ni wazo zuri, kutoweka kabisa apps hizi kwenye Playbook kunaifanya Playbook kupungua maana kwa watumiaji wa simu ambazo si Blackberry. Kwa upande wa watumiaji wa Blackberry, baada ya kuijaribu huduma hii tumegundua kwamba baadhi ya wakati huwa apps hizi hazifanya kazi kwa ufanisi, huwa zina kasi isiyoridhisha, huenda hili linasababishwa na ukweli kwamba Playbook na Simu ya BB huunganishwa kwa teknolojia ya bluetooth. wengi tunafahamu kuwa mawasiliano kwa njia hii si yenye kasi kubwa. 
Playbook itabaki kuwa mfungwa wa simu za BB mpaka RIM watakapotimiza ahadi ya kuweka apps muhimu zilizo kwenye BB Bridge
Afisa Mtendaji Mkuu mwenza wa RIM, Mike Lazaridis  ameahidi kuwa RIM wataweka apps hizi kwenye Playbook watakapofanya uboreshwaji wa OS yake, mpaka ahadi hii itakapotimia, hili linabaki kuwa ni kasoro ya kukosa apps muhimu kabisa, yaani ni jambo ambalo si la kufikirika katika Ulimwengu wa leo kuwa una tablet lakini huwezi huna contacts au inabidi email uangalie kwenye browser ya kawaida badala ya app maalum.

Simu Kupima Malaria

 

Wataalam katika Chuo Kikuu cha Carlifonia wamo katika harakati za kutengeneza chip ambayo itawekwa kwenye simu na kuwa na uwezo ya kugundua vijidudu vya Malaria kwenye mwili wa binadamu. Wanasayansi wawili wa Chuo hicho Peter Lilhoj na Chih-Ming Ho tayari wameshapata ruhusa ya kutengeneza kifaa hicho kutoka kwenye vyombo husika. Kifaa hicho kitakuwa kinatumika mara moja na kutupwa (disposable) na hivyo bila ya shaka kitakuwa ni kifaa cha kuchomeka tu badala ya kutengenezwa ndani ya simu. Kitakuwa kinafanana na kadi ya sim, kwa hiyo ni watumaini yetu kuwa kitatumika kwenye nafasi ya kadi kwa maana ya kwamba hakutakuwa na simu maalum yenye kufanya kazi hii, bali ni simu zote.

Wakati wametuacha bado tukitafakari ni vipi simu itapima na kugundua kilichopo kwenye damu, wataalam hao wameeleza kuwa lengo  la mradi huu ni kurahisisha na kusambaza upimaji na ugunduaji mapema wa maradhi haya ambayo mpaka sasa yameshateketeza maisha wa watu wengi mno Duniani na hasa katika nchi zilizoko Amerika ya Kusini, Afrika na Bara Hindi. Mradi huu unategemea kuanza kutumika nchini Msumbiji katika maeneo ya vijijini mara tu baada ya kukamilika kwa utengenezajiwa kifaa hichi. Bila shaka hii italeta faraja kubwa katika kuigundua Malaria hata hivyo matibabu hayatabadilika. Chuo Kikuu cha Carlifonia hakikuthibitisha ni lini kifaa hichi kitakuwa tayari kutumika.

Hacker Geohot Aajiriwa na Facebook

 

Geohot, hacker maarufu aliyejailbrake iPhone ameajiriwa rasmi na Mark Zuckerburg, yaani Facebook. Hacker huyu ambaye pia aliwahi kushitakiwa na Sony kwa shughuli za uchakachuaji baada ya kuihack PS3 na kuruhusu watumiaji kuweza kutumia DVD feki za kuchakachua. Facebook hawakuthubitisha Geohot atafanya kazi gani kwenye kampuni hiyo. Hacker huyu ambaye anatumia majina mbali mbali katika shughuli zake pevu ikiwa ni pamoja na million75, mil, dream na hax0r ameshafanya fujo nyingi sana katika ulimwengu wa kompyuta. Kijana huyu kwa sasa ana umri wa miaka 22 tu.

Jina alilopewa na wazazi wake ni George Francis Hotz. Katika kazi za karibuni kabisa alizofanya hacker huyu ni kujailbraik iPhone na iPod Touch kwa kutumia njia aliyoiita Blackra1n na pia kuifungua (sim unlock) simu hiyo kwa njia aliyooiita blacksn0w.
Alipoihack PS3 Sony walimpandisha kizimbani, hata hivyo mwezi wa nne mwaka huu Sony na Geohot walikubaliana nje ya mahakama na hivyo Sony kufuta kesi ile. Geohot alipewa sharti la kuto-hack tena PS3 ili kufutiwa kesi hiyo, sharti ambalo alilikubali. Ajira hii kwa dogo huyu ni hasara kubwa kwa wachakachuaji kwani watakosa mengi pale atakapotingwa na kazi za Facebook. Hacker huyu huwa hana noma, baada ya kufanya mambo yake huyaweka wazi kabisa katika tovuti yake ambayo ni www.geohot.com 
Kwa sasa kwenye tovuti yake ameacha ujumbe mfupi wa ajabu, waweza kwenda kuangalia mwenyewe.

Matumizi 10 ya simu na Tablet

 

Steve Jobs, Afisa Mtendaji Mkuu wa Apple akizungumza katika uzinduzi wa iPad alisema tunaanza kuishi katika kipindi ambacho kompyuta (akimaanisha desktop na laptop) imeanza kupitwa na wakati (post computer era). Ingawa tablet si aina mpya ya kompyuta, lakini iPad imeleta mabadiliko makubwa juu ya vipi tablet iwe na itumike. Mwaka huu ikiwa tumeugawa nusu, tayari kuna tablet zaidi ya 100 mpya zilizotolewa na kampuni mbali mbali, zipo za rahisi kabisa kama ile iliyotolewa India ambayo inagharimu $25.00 tu, na pia zipo za ghali mno kama ile ya iPad ya dhahabu na almasi ambayo imeuzwa Mamilioni ya dola.  Zipo zenye maudhi kwa kukosa ufanisi na pia zipo zenye maajabu kutokana na ufanisi wa hali ya juu kabisa.  Kwa upande wa simu, katika miaka ya karibuni kumetokea mapinduzi makubwa ya simu kutokana na ushindani wa kibiashara, simu imekuwa na uwezo, kasi na utendaji karibu sawa na kompyuta. Kiujumla matumizi ya simu na tablet yanafanana sana, lakini pia kuna tofauti mbili za msingi. Awali tablet si simu na pili simu huwa na display ndogo. Haya ni baadhi tu ya matumizi ya gajeti hizi:-


1. Mawasiliano

Hii ndio kazi ya msingi kabisa. Simu ni kifaa cha mawasiliano, hufanya shughuli kama vile kupiga simu, kuandika na kusoma meseji, kusoma email na mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter na My Space, kwa upande wa simu, hili ni maarufu zaidi kwa watumiaji wa Blackberry ambapo wengi tayari ni wagonjwa (addicted) katika matumizi ya Blackberry Messenger (BBM). Huduma kama hizi zinaonekana kutanuka zaidi ambapo iPhone nayo inategemewa kuanza huduma za iMessage miezi michache ijayo. Hata hivyo tablet inaonekana kuwa ni kifaa bora zaidi kwa kusoma mitandao jamii wakati simu ni bora zaidi kwa kuchangia kwa vile wengi wana kasi ya kuandika katika simu kuliko tablet.

2. Games
Simu hutumika kuchezea michezo (games) mbali mbali kama vile Angry Birds na Neeed For Speed. Kutumia games kwenye simu kumeongezeka zaidi katika miaka minne iliyopita hasa baada ya iPhone na Android kuingia kwa nguvu zote katika uwanja huu. Watabiri wengi wa mambo ya gajeti wanauona Ulimwengu wa baadae katika games kuwa upo kwenye tableti na simu za mkononi. Kwa upande wa tablet games nazo zinashamiri kwa kasi ya ajabu. Kwa mfano tablet yenye uhaba mkubwa wa apps, Blackberry Playbook imetoka ikiwa tayari ina game maarufu ya magari Need For Speed. Kampuni kubwa za games kama vile EA Sports na Unreal Technology wanashiriki kikamilifu katika kutoa games katika vifaa hivi. Cha kufurahisha zaidi ni kwamba games katika platfomu ya tablet na simu zinauzwa bei rahisi mno kulinganisha na Konsoli kama vile PS3 na Wii.

3. Msaidizi
Simu hutumika kama sekretari wa digital yaani kukukumbusha mambo mbali mbali, ikiwemo miadi (reminders), kazi mbali mbali (tasks), memo na mambo kama haya. Simu imekuwa ni kifaa maarufu cha kuamsha wale wenye kuamka mapema kwa sababu za kikazi au sababu nyingine. Hapa simu na hata tablet huonekana kama muokozi na msaidizi mkubwa katika maisha muhimu badala ya kifaa cha kujiburudiashia na mawasiliano tu.

4. Kusoma vitabu
Ingawa hili bado sio maarufu sana, wengine hutumia simu zao kusomea vitabu (ebooks) na hasa watumiaji wa iOS na Android. Hii imeletwa na iPhone pale walipoingiza app ya iBooks. Tablet kwa upande mwingine inaonekana kuwa ndio kifaa sahihi kabisa kwa shughuli za kusomea vitabu, kiasi kwamba soko la ebook readers limeingia mashakani mno kwa vile tablet mbali ya kusomea vitabu ina kazi nyingi zaidi. Hata hivyo kwa wale wenye kujali afya za macho yao wameendelea kutumia ebook reader kwa kusomea vitabu kwa vile diplay za ebook readers kama vile Kindle na Kobo hazina mwangaza.

5. Video calling
Hii ni huduma ambayo zaidi inategemea mtandao. Ingawa wengi wanadhani kwamba badi haiatumika ipasavyo tayari ipo katika platfomu mbali mbali kama vile iOS, Windows, Blackberry na Android. Huduma hii bado inatarajiwa kukua zaidi hapo miaka ya baadae. Huduma maarufu zaidi katika Vidoe calling ni Skype.

6. Kutembelea Tovuti
Hili kimsingi ni lenye kuvutia wengi zaidi, ambapo kampuni nyingi hasa katika nchi nilizoendelea zimekuwa zikiwabana watumiaji kwa kuwawekea kiwango maalum kinachoruhusiwa, kwa sasa wengi huruhusu baina ya 500 MB mpaka 1 GB kwa mwezi. Si kwenye tablet wala kwenye simu wengi wamekuwa wakitumia mtandao katika vifaa vyao, wengine hata bila ya kujali gharama.

7. Multimedia
Kupiga picha, kuzihifadhi, kurekodi video na kusikiliza muziki ni seheme ya maisha ya mwanadamu katika matumizi ya simu na tablet. Wengine hata wamefikia hatua ya kuangalia movie kamili kabisa na hasa kwa upande wa tablet ambazo ukubwa wa display ni kivutio katika multimedia.

8. Kupakua na kupakia
Hii ni sehemu yenye kuvutia mno, watu hupakua na kupakia mafaili kama vile ya muziki, video, picha na hata programu (apps) mbali mbali.

9. Kusoma habari
Kwa upande wa habari, hata watoa habari huchukulia tablet kuwa ni kifaa chenye kufaa zaidi. Magazeti mengi katika nchi zilizoendelea kama vile New York Times, The Times na The Sun tayari yanapatikana katika tablet na hata simu. Vile vile majarida makubwa kama Financial Times na The Economist hupatikana katika tablet mbali mbali na hasa iPad. Pia kuna majarida ya burudani, vichekesho na mafunzo mbali mbali. Mashirika ya habari makubwa yamekuwa wakiweka TV za live kwa njia ya streaming katika vifaa hivyo. Sky News, BBC na CNN zote zinapatikana kwenye tablet na simu.

 10. Kazi za Kiofisi
Kwa vile simu na tablet huja na Word processors, Spreadsheets, Database na presentation app, na vile vile kuna vifaa kama Blackberry vyenye usalama wa hali ya juu wengine wamekuwa wakifanya kazi za kiofisi katika vifaa hivi.

Ingawa haya si matumizi pekee ya vifaa hivi wengi hufanya mengi kati ya haya, lakini pia huu sio mwisho, uvumbuzi bado unaendelea, teknolojia kama GPS, acceletrometer, Gyroscope na digital compass tayari zimeshaleta matumizi mengi ya ziada katika vifaa hivi. Katika makala zijazo tunatarajia kuzungumzia matumizi ya simu katika siku za baadae.

Archos na Simu ya Ndani Yenye Android

 

Kampuni ya Ufaransa, Archos walitoa tablet muda mrefu kabla ya Apple kutoa iPad, ilikuwa ni tablet ya kwanza kutumia Windows 7. Kwa mara nyingine Archos imezitangulia kampuni nyingine kwa kutoa simu ya ndani (landline) inayotumia OS ya Android, hebu vuta fikra; unacheza Angry Birds kwenye simu ya ndani halafu unatumia skype, unasoma na kujibu email zako kisha unafanya video calling, hapo bado huna bili hata ya senti moja katika simu, ni intanet tu ndio inayofanya kazi. Simu hii inatumia protocol za DECT za kawaida na hivyo kuiwezesha kuunganisha kwenye line ya ADSL. La kuvutia zaidi katika simu hii ni kwamba Android market inapatikana, kwa hiyo una nafasi ya kuchagua apps zozote unazotaka kati ya laki tatu zilizopo kwenye soko hilo. Archos wameiita simu hii Archos 3.5 Smart Home Phone.

Jee huu utakuwa ni mwanzo wa ukiritimba wa Google katika simu za ndani? Tayari 48% ya simu za mkononi zinaendesha na OS ya Android inayotolewa na Google. Hii imezifanya simu zilizokataa kutumia OS hiyo ukiondoa  iPhone, kama vile Nokia karibu kusahauliwa katika soko la simu za hali ya juu, ingawa kwa sasa Windows Phone imetoa matumaini mapya kwa wale walioikataa Android.
Simu hii ina display yenye ukubwa wa 3.5” ikiwa na skrini ya kugusa. Huenda hii ikawa ni smartphone ya kwanza kuwa ni simu ya ndani. Inafanana kimaumbile na bidhaa nyingine za Archos na imetengenezwa na dock ambayo ndio yenye kuunganishwa na line ya simu, ukutani. Simu hii pia ina kamera yenye uwezo wa kurekodi video za HD katika kiwango cha 720p, ambapo maana yake ni kwamba unaweza kufanya high definition video calling. Archos hawakutoa tarehe ya kuanza mauzo ya simu hii wala bei yake, lakini inatarajiwa kuuzwa Faranga za Kifaransa nyingi tu ukilinganisha na simu nyingine za ndani. Kaa mkao wa kula mapinduzi katika simu za ndani yameanzia hapa.

Mtego wa Mbu, Eneo la Eka 1

 

Hebu fikiria ukinunua huu mtego sio tu utakuwa umejikinga wewe na watu wa nyumba yako na mbu bali huenda ukawa umeunusuru mtaa mzima na malaria, adha ya sauti za mbu  pamoja na vijipele vya kutafunwa nao. Dynatrap imetengenezwa maalum kwa ajili ya matumizi ya nje badala ya ndani ya nyumba kwa hiyo kwa wale wapanda milima, wakaa maskani, waweka kambi na kadhalika wao hasa ndio walengwa wa Dynatrap.  Hata hivyo kwa matumizi ya nyumbani inafaa kwa zile nyumba zilizozungushiwa uzio.  

Dynatrap ina taa aina ya florecent mbili ambazo huzalisha moinzi ya ultraviolet, mionzi hii hukutanishwa na gamba aina ya titanium dioxiding liliwekwa kwenye mtego huu na hivyo mchanganyiko huu huzalisha gesi aina ya carbon dioxide ambayo ndio hasa inayowavutia mbu na baadhi ya videde vingine vinavyoruka, harufu itokayo katika kijigajeti hichi ni sawa na ile ya binadamu anapopumua na kutoa gesi ya CO2 ambayo wadudu hawa ndio huvutika nayo.
Sasa ni vipi mbu au wadudu wengine hunaswa na mtego huu baada ya kuvutika na harufu hii? Dynatrap ina kijifeni fulani ambacho kina nguvu za kutosha cha kuwavuta wadudu wanapoikaribia, baada ya kuvutwa huingizwa kwenye neti ambapo hubaki humo mpaka wanapokufa. Ingawa kuna mitego mingi ya namna hii lakini kilichotuvutia kwenye mtego huu ni ule uwezo wa kuvutia wadudu katika eneo la mraba la eka nzima. Pia kivutio chengine ni kule kutokutumia kemikali zozote ambazo kwa kawaida hutoa athari fulani ama kwenye mazingira au binadamu mwenyewe. Bei ya mtego huu ndio tatizo, ni $199.95 za Marekani sio za Zimbabwe. Iwapo unataka kuuagiza mtego huu jina lake kamili ni One Acre Natural Attractant Mosquito Trap. Kama hizi fedha ni nyingi unaweza kujaribu kupigisha donation mtaani. Ni wazo tu.

Blogi ya habari huru zisizo na upendeleo na uchambuzi yakinifu kuhusu Gajeti na Teknolojia Duniani