Nokia N9 yatinga na Meego OS

Mbali na kutangaza wazi kuwa wanajiunga na Windows Phone 7 sasa Nokia wamekuja na kifaa sio cha kawaida kikiwa kinatumia OS ya MeeGo. Hii inadhihirisha wazi dhamira ya Nokia kuachana kabisa na Symbian OS. Nokia wamechelewa mno katika uamuzi huu, kampuni zote nyingine ikiwa ni pamoja na Samsung, Life is Good (LG) na Sony Ericsson wameachana na OS ya Symbian kwa muda mrefu sasa. Hata hivyo kutumia kwao MeeGo OS pia kunaonyesha ni wazi kuwa Nokia walikuwa na dhamira ya kupambana na Android ya Google. MeeGo na Android ni OS zenye asili ya Linux, OS  ya MeeGo inaendelezwa kwa ushirikiano wa Nokia na Intel baada ya kampuni hizo kuunganisha juhudi zao za zamani katika OS ambazo ni Moblin ya Intel na Maemo ya Nokia. Simu hii itajulikana kama Nokia N9. Hata hivyo MeeGo OS bado ni changa kwani imetangazwa mwaka 2010. Nokia N9 itakuwa ni simu ya kwanza kutumia MeeGo OS lakini pia huenda ikawa ni ya mwisho kwa ule maktaba wa Nokia kutumia Windows Phone 7

Umbile la Nokia N9 ni lenye kuvutia mno machoni, umbile ambalo tunaweza kuliita jipya kwani hakuna simu inayofanana na Nokia hiyo. La kwanza kabisa ni kwamba simu hiyo haina hata kifungo (button) kimoja mbele. Vianisho halisi vya simu hiyo ni vya hali ya juu, ni wazi kwamba Nokia wamekuja na hasira wakitaka kurudi mchezoni na kutambulika kama zamani. Vianisho halisi hivyo: 
RAM: Gigabyte moja, hii inaonekana kama ni jambo la kawaida kwa sasa kwani simu zote  ambazo ni za kiwango cha juu zina RAM hii. Hata hivyo gigabyte moja inatosha kabisa kuifanya simu kufanya kazi kwa ufanisi. 
Diplay: ina ukubwa wa 3.9” ikiwa na mvimbo wa aina fulani (Concave), imeizidi iPhone 4 kwa 0.4”, ni muhimu kufahamu kuwa simu zote ambazo huwa katika simu bora zina display yenye ukubwa kati ya 3.5” na 4.3”
Prosesa: Ina kasi ya gigabyte nzima, sawa na ile iliyotumika kwenye Samsung Galaxy S2 ambayo wengi wanaiona kama ni simu bora kwa sasa. 
Hard Drive: Simu hiyo pia ina drive aina solid state (SSD) yenye ukubwa kuanzia gigabyte 16 hadi 64, iPhone imeishia 32GB na hivyo hii inaifanya Nokia hii kuwa ni simu yenye drive ya ndani kubwa zaidi kuliko simu zote.
Kamera: ina megapikseli 8 pamoja na lenzi aina ya Karl Seiss ambayo hutumika sana kwenye kamera aina ya Sony. Kamera hiyo pia ina flashi na uwezo wa kurekodi video za HD katika kiwango cha 1080p kamili. 
Ikiwa hujatosheka na ubora wa hali ya juu wa vianisho hivi simu hii pia itakuwa ni ya kwanza kuwa na teknolojia ya Dolby Digital Plus pamoja na Dolby headphones post prosessing ambayo itakufanya usikie sauti safi na kali aina ya surround. Pia simu hiyo itatumia Micro Sim kama zile zilizotumika kwenye iPhone 4 na iPad zote zenye 3G. Nokia N9 pia ina Near Field Technology (NFC) ambayo itaiwezesha simu hiyo kusoma habari mbali mbali za digital kama vile kulipa supermarket baada ya simu hiyo kuingizwa tarakimu zote zinazohusiana na akaunti yako ya fedha. Simu hii pia ina GPS.
Simu hiyo itakapotolewa itakuwa tayari ina baadhi ya games ambazo ni maarufu ikiwa ni pamoja na Angry Birds, Galaxy on Fire 2 na Real Golf 2011.  Sisi katika Gajetek tunadhani kuwa simu hii itakapotolewa itakuwa na nafasi nzuri ya kukaa kwenye simu kumi bora Duniani, angalau kwa muda mchache, hii pia itategemea na simu nyingine mpya zitakuwa vipi. Pia bila ya shaka yoyote OS ya MeeGo italeta mapinduzi mapya katika simu za mkononi. Kasoro kubwa katika OS hii itakuwa ni uchache wa apps kama ilivyo kwenye OS yoyote mpya. Hata hivyo kuna uvumi kwamba katika makubaliano ya Nokia na Microsoft kujiunga na kambi ya Windows Phone, Nokia watalazimika kuacha kuiendeleza MeeGo OS, ikiwa hili ni kweli hizi ni habari za kusikitisha, kwani wateja ni bora kwao kuwe na nafasi ya kuchagua baina ya OS mbali mbali na hivyo kuondoa uwezekano wa ukiritimba katika soko. Hata hivyo ni kwa nini Nokia watumie OS ambayo ni miezi michache ijayo inabidi kuachana nayo? Haya ni mambo ya kushangaza kwa upande wa mikakati ya Nokia, kampuni ambayo imepoteza hisa kubwa katika mauzo ya simu Duniani baada ya kuingia kwa Android na iPhone, takriban miaka mitano iliyopita. 

Leave a comment