iPad 2 ya Bilioni 12!

Stuart Hughes na iPad yake, haoni hatari
kuuza  chochote hata kwa mabilioni.

Tunaishi katika Dunia ya ajabu, wengi tunajituma kufanya kazi masaa 40 au zaidi kwa kila wiki maishani mwetu ili kutafuta pesa tukidhi mahitaji yetu, lakini pia wako wanaoishi na wanatafuta namna ya kutumia fedha kwani kwao wao zimekuwa nyingi mno na zinawatatiza. Mapema mwaka huu sonara Stuart Hughes ameingia katika kitabu cha rekodi za Dunia (Guiness World Record 2011) kwa kuuza iPad kwa jumla ya £ 109,995.00 (Sawa na TSh 278,998,208.00), ni sawa kabisa hatujakosea milioni 278!. 

iPad hii aliita Stuart Hughes Supreme Gold Edition iPad ambayo ina gamba la dhahabu ya kareti 22. Pia nembo ya Apple katika iPad hii imetengenezwa kwa almasi ambapo imewekwa mawe 53 yenye kareti 25.5, tunaomba kuwajulisha kwamba aliyenunua iPad hii si mwendawazimu.
iPad ya dhahabu ikiwa na nembo ya almasi
Kama bado hujashikwa na mshangao Stuart Hughes ameshusha iPad 2 kwa bei ambayoha kushangaza kuliko ya Stuart Hughes Supreme Gold Edition iPad. Kabla ya bei iPad 2 hii ina uzito wa kilo mbili nayo vile vile imewekewa gamba kwa dhahabu na logo ya Apple ya almasi. Pia hii kwa sehemu ya mbele imepambwa kwa mfupa wa dainasoo ambao umefanyiwa mchaganyiko maalum, mfupa huo unaaminika kuwa umetokana na dainasoo aliyeishi miaka milioni 65 iliyopita. Bei ya gajet hiyo iliyopewa jina la iPad 2 Gold History Edition ni TSh 12,682,312,704.00 (£5,000,000.00) Stuart Hughes mwenyewe amekiri kwamba yeye huyafanyia kazi yale mawazo ambayo ni ya kiwazimu, akimaanisha kuwa hauzi kwa bei za kawaida. Aliwachekesha watu aliposema kuwa yeye hupunguza bei (discount) hadi kwa 30%
Mbali na bidhaa hii, Stuart Hughes pia ametengeza Blackberry Bold 9700, iPhone na iPod Touch za dhahabu na almasi. Sonara huyu anaishi katika mji wa Liverpool nchini Uingereza. Iwapo una mpango ya kununua iPad 2  Gold History Edition inabidi ufanye fasta kwani zimetengezwa mbili tu.

Hatimae Sony kutoa Tablet

 

Wengi wanajiuliza ni kwa nini kampuni ya Sony imechelewa mno kwenye dimba la kompyuta za tablet. Hata hivyo kuna usemi ‘ni bora kuchelewa kuliko kukosa kabisa’. Sony wametangaza kwamba wanatarajia kutoa tablet mbili kwa pamoja katika kipindi cha mwisho wa mwaka. Tablet hizo zitajulikana kama Sony S1 na Sony S2.

Kikubwa kabisa Sony pia wamebwaga manyanga na kuamua kujiunga na kambi ya Android badala ya kutengeza OS yao wenyewe. Hii si kawaida ya Sony ukuzingatia wanatumia OS zao wenyewe kwenye Plasytation 3 naPlaystation Portable (PSP). Toleo la Android litakalotumika katika tablet hizi ni Honeycomb 3.0 kutoka Google, maalum kwa ajili ya tablet. 
  
Sony S1
Sony S1 itakuwa na skrini yenye ukubwa wa inchi 9.4 na S2 itakuwa na skrini mbili (kama zile za Acer Iconia), kila moja kati ya skrini hizo zina ukubwa wa inchi 5.5, Sony S2 itakuwa inafungika namna ya unavyofunga kitabu. Prosesa ambazo Sony wametangaza watatumia ni Dual Core bila ya kuanisha kasi au aina ya prosesa zenyewe. Tablet zote mbili zitatoka na Wi Fi, 3G pamoja na remote za kuendesha TV za Sony , bila ya shaka tunatarajia tablet hizi zitakuwa na mahusiano na maingiliano kwa namna fulani na vifaa vingine vya Sony kama vile TV, PS3, PSP na simu za Sony Ericsson ambazo nazo tayari zinatumia OS ya Android.
Sony S2
Kadhalika Sony wamewahakikishia wateja wao kwamba Tablet zote mbili zitakuwa na huduma ya Qroicity Music na E Reader za Sony, hali hii inazidi kutia mashaka juu ya mustakbali wa E – Readers, ambao wengi wametabiri kutoweka kwa gajet hizi hasa baada ya kuwepo kwa tablet, kwa vile kazi yake inafanywa pia na tablet. Akizungumza kuhusu tablet hizi Naibu Rais wa Bidhaa na Huduma za Sony, Kunimasa Suzuki amesema tablet hizi zitakuwa ni za kipekee kwani zitaunganisha vifaa hivi na huduma nyingi za mtandaoni za Sony. 
Washabiki wengi wa gajet wanazisubiri kwa hamu tablet hizi ambazo zinaonekana kuwa ni zenye kuvutia kwa namna zinavyoonekana, ni miezi michache imebaki, jee tablet hii itaweza kutoa ipinzani wa kweli kwa iPad 2? iPad 2 ndio kinara wa tablet zote mpaka sasa.

Evo 2 ‘Game Console’ mpya

 

Kampuni ya Envizions imejitosa kwenye vita vya michezo ya kompyuta dhidi ya kampuni kubwa za Sony, Nintendo na Microsoft zinazotengeneza kompyuta za michezo za Playstation 3, Wii na Xbox 360. Envizions wameamua kujiingiza katika biashara kwa kutoa kompyuta itkayokuwa inatumia platfomu ya Android ambayo ni open source, iwapo kampuni hii itafanikiwa kuingia vyema katika uwanja huu huenda ikaharibu biashara za kampuni hizi nyinginezo, hili tutalijadili mbele.

Kwa upande wa vianisho halisi kompyuta ya michezo hii itatumia prosesa yenye kasi ya Ghz 1.2 ambayo hawakuitaja ni ya aina gani, hat hivyo wamedokeza kuwa itatengezwa na kampuni ya Korea ya Kusini, Samsung. Evo 2 itatumia OS ya Google, aina ya Android  Froyo 2.2 lakini wameahidi kuwa itafanyiwa mabadiliko makubwa ili kuiwezesha kukidhi mahitaji ya kompyuta hii, mpaka sasa Android hutumika tu kwenye simu na tablet, ingawa wako waliojaribu ku-boot kompyuta za kawaida kwa kutumia OS hiyo.
Kwa upande wa vikorokoro, (Console) konsoli hiyo itauzwa na rimoti ya mabox ya Evo TV pamoja na kontrola ya game yenyewe. Vile vile itakuwa na waya wa HDMI ambapo hii inamaanisha kwamba itakuwa na HDMI port. Kampuni hii pia imetangaza kuwa wanalengo la kutumia teknolojia ya 3D motion sensor ambapo sdk yake kwa watengenezaji wa games itatoka wiki chache zijazo.
Turudi kwenye hoja yetu huko juu, ni vipi wanaweza kuharibu biashara za game kwa kampuni kubwa ambazo tayari zinazuza mamilioni ya kompyuta hizo. Kwanza kabisa Android tayari imevutia watengenezaji  game (developers) wengi mno kwa hiyo maana yake ni kwamba kutakuwa na chaguo la game nyingi mbali mbali katika konsoli ya Evo 2 na hivyo kutoa ushindani. Android ni maarufu pia kwa kuuza Apps kwa bei rahisi, kwa wastani ni £2.00 (TSh 5,105.00) tofauti na software za Xbox, Wii na PS3 ambazo kwa wastani huuzwa £30.00 (Tsh 76,584.00), hatutegemea kwamba Envizions watauza game kwa £2.00 lakini iwapo wataweka mkakati wa kuuza bei ya chini zaidi ya wapinzani ni wazi watawalazimisha watengeza game nyingine nao washushe bei za game zao, pia itawafanya wapate share ya kutosha katika mauzo.
Tayari Android ina game maarufu kama vile FIFA, PES na Need For Speed. Kwa hiyo hii itawawezesha kujikita katika uwanja huu kwa haraka na hivyo kutoa upinzani wa kweli kwa kampuni kubwa hizo. Hata hivyo wanahitaji kufanya uvumbuzi wa hali ya juu ili kuvutia wateja ukizingatia vifaa vyenye kutumia motion sensor na sensor za kamera kama vile kinect ya Xbox 360 ndio vinavyovutia zaidi wachezaji wa michezo hiii kwa sasa. 
Envizions tayari imeshaanza kusajili developers kwa ada ya $150.00 (£91.00 au TSh 232,306.00) kwa mwaka na wametangaza kuwa konsoli hiyo itakuwa tayari kwa mauzo itakapofika kipindi cha kiangazi mwaka huu, miezi michache kutoka sasa. WAtakaojisajili watapatiwa komyuta moja kwa ajili ya kujaribia game watazozitengeneza. Evo 2 itauzwa kwa $250.00 ambapo tunadhani hii huenda itapunguza kasi ya mauzo ya konsoli hiyo. Ni wazi kuwa Envizions wanaingia katika soko hilo wakilenga kuwa na sifa ya kuwa ni miongoni mwa konsoli za hali ya juu.

Toshiba Yashusha Qosmio ya Nguvu

 

Qosmio ni laptop zilizotamba sana katika miaka ya tisini mwishoni, hata kabla ya Sony Viao kuingia dimba la laptop kwa kasi. Toshiba wamejitutumua tena mara nyingine na kushuka na Qosmio X770 laptop yenye vianisho halisi balaa. 
Laptop hii inaendeshwa na prosesa aina ya iCore7 2630QM, ikiwa pia na kadi ya graphics aina ya NVIDIA GeForce GTX 560M yenye memory 1.5 GB, laptop hii inawafaa wenye kucheza michezo ya kompyuta na mambo mengine ambayo yanahitaji graphics nyingi. Pia laptop hii ina RAM GB 8 aina ya DDR. 
Qosmio X770 ina skrini yenye ukubwa wa ichi 17.3 na rezolushan zake ni 1920×1080. Hard Drive ina ukubwa wa 1.25 Tetrabyte. Vile vile laptop hii ina kamera yenye HD na 3D pia huuzwa pamoja na miwani yake maalum kwa ajili ya 3D. Kibei inabidi ujitutumue kidogo kwani itakapokuwa madukani bei itasomeka $1,850.00 (sawa na TSh 2,861,025.00) Laptop hii inategemewa kuingia madukani wiki chache zijazo. 

XBox 360 Bwaaa kwa mara nyingine!

 

Baadhi ya XBox 360, gajet ya michezo ya kompyuta inayotengenezwa na Microsoft zimekorofisha tena, miaka ya nyuma XBox ilisumbuwa sana wateja wake kwa kile kilichokuja kujulikana kama “Red Ring of Death” maarufu kwa ufupisho wake RROD. Microsoft wametatua tatizo hili moja kwa moja ingawa lilichukua muda mrefu na kuwachanganya pamoja na kuwaiudhi wengi kwani RROD ilimaanisha mwisho wa gajet yako, ingawa watundu wachache waliweza kulitatua tatizo hili. 
Hivi karibuni Microsoft wameboresha software ya kifaa chao hicho. Kuboreshwa huko kwa software kunalenga kuzuia wale wanaotumia ‘disk feki’. Matokeo yake ni kwamba baadhi ya Xbox 360 zimepoteza uwezo wa kusoma disk mpya aina ya XGD3 zinazotumika katika gajet hii. Hii inadhihirisha kuwa gajet hii bado haina umadhubuti unaotarajiwa na wateja kutoka kampuni kubwa kama Microsoft.

Hata hivyo Microsoft wamechukua hatua za kistaarabu kabisa, wamekiri kuwepo kwa tatizo hili. Pia Microsoft wametoa ‘ofa’ kwa yeyote mwenye tatizo hili atapatiwa Xbox 360 mpya ya bure, sharti arudishe ya zamani. Hii huenda ikawaokoa Microsoft kuharibu mahusiano mazuri na wateja wake. Hata hivyo Microsoft wamedai kuwa tatizo hili limewaathiri watuamiaji wachache tu yaani chini ya 10,000 kati ya milioni 50 wanaotumia gejet hii. Xbox mpya wanazopewa waathirika ni zile zenye GB 250.
Hii itawapa nafuu kidogo Sony baada ya kashfa iliyoiharibia jina kampuni hiyo kwa kuvujisha vielelezo vya siri wachezaji wanacheza PS3 kwenye mtandao. Hata hivyo ingekuwa sisi wa Gajetek tuna nafasi ya kuwapa ushauri Microsoft tungewaambia waache mambo ya hardware kwani ni wazi huwa yanawasumbua sana na biashara yao iendelee kuwa pale walipopata mafanikio makubwa yaani kwenye software. Huu hapa ushahidi chungulia mwenyewe, kimombo hicho:-

LG Optimus Pad; Tablet yenye 3D

 

LG Optimus Pad ukipenda T Mobile G Slate
‘Life is Good’ maarufu zaidi kama LG wanadhihirisha kuwa bado wamo mchezoni katika Ulimwengu wa gajet, miezi michache iliyopita LG ilikuwa ni kampuni ya kwanza kutoa simu yenye prosesa ambayo ina core mbili. Leo tunachambua gajet nyingine ambayo imetolewa na LG nayo ni tablet ijulikanayo kama LG Optimus Pad, tablet hii ni ya kwanza kuwa na kamera yenye 3D.

Kabla kuzungumzia 3D kwanza tuangalie vianisho halisi vya tablet hii. Inatumia Android Honeycomb 3.0 iliyotolewa na Google.Optimus Pad ina skrini yenye ukubwa wa inchi 8.9 aina ya capacitive yenye uwezo wa multitouch. Skrini hii ina piksel 1,280×768. Pia ina uzito wa gramu 630. Optimus Pad inaendeshwa na NVIDIA Tegra 2 dual-core yenye kasi ya Ghz Moja. Kwa vile prosesa hii ina core mbili huiwezesha tablet hii kufanya kazi kwa ufanisi mzuri. 

Kamera 2 zinazorekodi kiwango cha 3D
Kwenye suala la kamera LG wamegongemelea msumari na hapa ndipo LG walipolenga kuwa ni kivutio cha mauzo. Optimus pad ina kamera mbili nyuma, kila moja ina megpiksel 5 ambapo utaweza kutengeneza ‘Avatar movie’ yako mwenyewe katika kiwango cha 3D. Kamera hii hata hivyo unahitaji sehemu yenye mwangaza wa kutosha la sivyo huwa inatoa picha yenye giza kiasi fulani. Kamera mbili hizi pia hurekodi video za HD katika kiwango cha 1080p. Kamera ya tatu katika pad hii ni iliyoko mbeleni na ni web cam ya kawaida tu kwa ajili ya kuchati.
Skrini ya Optimus pad haina uwezo wa kuonesha picha za 3D. hivyo basi tablet hii inabidi uunganishe na TV yenye 3D kwa kutumia port ya HDMI. Hata hivyo iwapo utatumia miwani za 3D zenye kioo kimoja cha bluu na cha pili chekundu,  itakuwezesha kuona 3D lakini si kwa ukamilifu. 
Huko marekani tablet hii imepewa jina la T Mobile G slate ambapo imeshushwa ikiwa na teknolojia ya 4G, teknolojia ambayo katika bara la Ulaya inategemea kuanza kutumika mwaka 2012.
Kwa ufupisho, vigezo vinavyoifanya tabet hii kuwa miongoni mwa tablet bora ni kamera yenye kurekodi 3D na HD ikiwa na piksel 5, Dual Core Prosesa yenye Ghz 1, Android Honeycomb ya Google na kwa waliopo Marekani teknolojia ya 4G. Vinavyoiangusha tablet hii ni bei ambapo huuzwa $750.00 (sawa na Tsh 1,160,000.00) na kukosa skrini yenye kuweza kuonesha video za 3D, maana yake ni kwamba kama huna TV ya 3D ni vyema ufikirie kununua tablet nyingine. Hatuna uhakika kama kuifanya tablet hii kuwa na ukubwa tofauti na tablet nyingi yaani inchi 9 kutaisaidia kupata wateja kampuni ya Maisha ni Mazuri (LG), kwa vile tablet zote zina kambi mbili yaani ya inchi 10 na kambi ya inchi 7.

Sony watangaza headphones mpya za PS3

 

Kampuni inayotengeneza michezo ya kompyuta ya Playstation, Sony, wametangaza na kuonesha headphone mpya ambazo zitaanza kuuzwa mwezi septemba mwaka huu. Sony ambao sasa ni wazalishaji wa bidhaa mbali mbali za electroniki wametangaza bei ya gajet hiyo kuwa ni $100. (TSh 154,605.00) kwa moja tu. Kwa watoto wenye kujinunulia wenyewe yafaa waanze kuchanga fedha hizo tangu sasa.

Headphone hizo hazitumii waya bali huja na kufaa kinachopachikwa katika USB port ya PS3 ili kuwasiliana. Pia headphones hizi zitakuwa zinatoa joto fulani kwa vile zitatolewa katika kipindi cha baridi. Kwa wanaoishi nchi za joto basi headphones hizi hazifai laa sivyo ukae na feni au kiyoyozi.

Pia headphone hizi zina kipaza sauti kwa ajili ya kuchati na mpinzani wako unapocheza game za kwenye mtandao. Vipaza sauti hivyo vina kifungo cha kuongeza na kupunguza sauti, pia unaweza kuzima kabisa sauti ya unaezungumza nae na kubaki na sauti ya game tu.
Headphones hizo zina teknolojia ya surround sound 7.1 ambapo sauti yake ni sawa na kuweka spika saba pamoja na subwoofer katika chumba kimoja. Kwa watakaonunua angali usije ukaathirika masikio. Hata hivyo zinatarajiwa kuwa na sauti safi na sauti kubwa kuliko ile ya Phillips!

BMW Washusa ‘Kitu na Box’

 

Gari dhana iliyotengenezwa na kampuni ya BMW
Hii si gari katika sinema ya iRobot. Hii ni gari ya dhana (concept car) ambayo imetengezwa na kampuni yenye kutengeneza magari ya kifakhari BMW. Wengi wetu bado hatujaweza hata kuifikiria kuhusu mambo yatakayokuwemo katika gari hii hapo uzalishaji wa kibiashara utakapoanza. Ikiwa ni mchanganyiko wa burudani, faraja, usalama na mawasiliano ya hali ya juu, gari hii imezungukwa na vihisia (sensors) kila upande na kujaa teknolojia ya robot pamoja na kamera. Imejengwa kwa utaalamu na ufanisi wa hali ya juu. 
Kwa kutumia vihisia na kompyuta iliyopo kwenye dashbodi, vioo vya pembeni humpasha habari dereva juu ya yanayojiri nje ya gari, kwa mfano kuna gari inayojaribu kuovateki. Taa zimefungwa pamoja na kamera zenye uwezo wa kugundua magari na vitu vingine na hivyo kumpasha habari dereva ambazo zitasaidia kuepusha ajali au hata gari kujipiga breki wenyewe.
Pia kompyuta ambayo ina mtandao humpasha habari muhimu dereva juu ya njia ambazo anaweza kupita au inabidi aziepuke kwa vile kuna msururu wa magari uliokwama. Abiria nae ana televisheni iliyounganishwa na kamera  iliyo nje itakayoweza kumuonesha sehemu zinazovutia nje ya gari. Pia televisheni hiyo au tuseme kompyuta ina mtandao kamili.
Dashibodi ya Gari dhana ya BMW na namna inavyoonekana kwa juu
Wakizungumza kuhusu gari hii ambayo BMW waliitoa kwenye maonesho ya gari yaliyofanyka huko Geneva, wataalam wa kampuni hiyo wamesema wako njiani kukamilisha utengeneza wa gari hii ili iwe tayari kwa uzalishaji wa kibiashara, wanalenga zaidi kuifanya gari hiyo iwe na usalama, upashaji habari mzuri pamoja na kuwaburudisha watumiaji. 

Ili kupata mauzo zaidi tunatumai kwamba BMW wataitengeneza gari hii iweze kuchukua angalau abiria wanne badala ya mmoja (pamoja na dereva) kama ilivyo hivi sasa, au kutoa aina zaidi ya moja mbali ya hii aina ya ‘sports’. Hata hivyo mbali na kuionesha BMW wameonekana kutokuwa tayari kutoa habari nyingi za gari hii ili kuepuka wapinzani wasije kuwapiku.

>Soka Na Teknolojia

>

Leo ni leo, asiye na mwana aelekee jiwe, ama Man U au Barca. Ni siku ya fainali ya ligi ya Mabingwa wa Ulaya ambapo mabingwa wa nchi mbili zinazotawala katika soka Duniani Uingereza na Uspanyola watapambana. Sisi katika Gajetek tunaangalia mchezo huu na teknolojia.
Chips za GPS katika Mpira wa Adidas. 
Teknolijia ya mstari wa goli, hii ni teknolojia ya kuwasaidia waamuzi kujua kama mpira umevuka mstari wa goli kwa hiyo goli limeingia au haukuvuka. Kwa muda mrefu sasa viongozi wa shirikisho la soka duniani FIFA kwa  nguvu zote wamekuwa suala la wakipinga teknolojia yoyote kutumika ili kumalizo mzozo huo ambapo mara kadhaa waamuzi hutoa uamuzi usio sahihi kama goli au si goli, kosa maarufu la namna hii ni lile lililofanyika katika Kombe la Dunia Afrika ya Kusini mwaka jana. Kiungo wa Uingereza Frank Lampard, alipopachika bao katika mechi dhidi ya Ujerumani na muamuzi alishindwa kujua kama mpira ulivuka chaki ya goli. 



Kwa nini Blatter na viongozi wenziwe wamekuwa wakipinga matumizi ya teknolojia kuwasaidia waamuzi katika suala hili? Wengi kati ya wapenzi wa mchezo huu maarufu Duniani kwa kweli hawakubaliani na hoja dhaifu anazotoa rais huyu wa shirikisho la soka, kama vile eti matumizi ya teknolojia yatapunguza ladha ya mchezo! Tuachane na Blatter ambaye huenda ana ajenda za siri katika hili, muhimu kwetu sisi ni teknolojia.

Teknolijia ya mstari wa goli ipo tayari, kinachosubiriwa ni FIFA kuidhinisha majaribio na hivyo iweze kutumika msimu ujao, hata hivyo FIFA bado hawajatoa kauli thabiti. Mipira itaingizwa kifaa cha GPS (Geographical Pisitioning System) ambacho kina uwezo wa kujua mahala ambapo mpira upo popote uwanjani kwa kutumia satalaiti maalum na kwenye mstari wa goli panawekwa lesser beam ambazo zina vihisia (sensor) vinavyoweza kuwasiliana na chip ya GPS iliyoko kwenywe mpira kwa hiyo iwapo mpira utavuka kwenye mstari wa goli lesser beam zitaweza kumjulisha muamuzi kuwa mpira umevuka chaki ya goli hivyo kuondoa makosa ya uamuzi katika suala hili.
Texaco Shinpads zenye sensors 
Mbali na teknolojia hii, hivi karibuni kampuni ya Texaco wametengeneza vikinga ugoko (Shinpads) vyenye uwezo wa kumjulisha muamuzi kama mchezaji amechezewa rafu au amejitupa. Vikinga ugoko hivyo vimewekewa vihisia (sensors) maalum ambavyo vinauwezo wa kutambua iwapo mchezaji amegongwa kweli au amejitupa tu. Iwapo amegongwa vihisia hivyo vitampelekea habari muamuzi kuwa rafu ni ya kweli, la kama hakugusana na mchezaji mwenziwe vihisia hivyo havitatoa mawasiliano yoyote na hivyo muamuzi atajua kwamba mchezaji amejitupa. Baadhi ya washambuliaji katika soka wamekuwa na tabia ya kujitupa katika boksi ya 18, ili kumhadaa mwamuzi kutoa penalti. Muamuzi mstaafu maarufu wa soka Uingereza Jeff Winter ameeleza kufurahishwa kwake kutokana na kutengenezwa kwa shinpads hizo kwa vile zitatoa msaada mkubwa kwa waamuzi. Je FIFA watazuia na hizi? 
Sisi katika Gajetek tunawatakia wapenda soka fainali njema, timu yetu ni itakayoshinda, hivyo tuna uhakika Mungu akipenda, timu yetu leo inachukua ubingwa. Ingawa mara nyingi inatubidi kubadili timu, faida yake ni kwamba mara zote tumo furahani. 

>10 Bora katika Twitter

>

1. Lady Gaga (@ladygaga)
Kazi: Mwanamuziki
Wanaomfuatilia: 10,423,381
Anaowafuatilia: 143,386
Obama; mwanasiasa pekee katika kumi bora
ya twitter

Idadi ya Twit alizoandika: 818


2 Justin Bieber (@justinbieber)
Kazi: Mwanamuziki
Wanaomfuatilia: 9,936,549
Anaowafuatilia: 113,469

Idadi ya Twit alizoandika: 9,246
3. Barack Obama (@BarackObama)
Kazi: Rais wa 44 wa USA


Wanaomfuatilia: 8,250,557
Anaowafuatilia: 696,945
Idadi ya Twit alizoandika: 1,357
4. Britney Spears (@britneyspears)

Kazi Mwanamuziki
Wanaomfuatilia: 7,988,551
Anaowafuatilia: 422,609
Idadi ya Twit alizoandika: 755
5. Kim Kardashian (@kimkardashian)
Kazi: Mfanyabiashara, Mbunifu wa Fashion, Mtangaza Manukato, Mwendeshaji wa kipindi cha Televisheni

Wanaomfuatilia: 7,636,684
Anaowafuatilia: 139
Idadi ya Twit alizoandika: 7670
6. Katy Perry (@katyperry)
Kazi: Mcheza sinema, mwandishi wa nyimbo.
Wanaomfuatilia: 7,519,007
Anaowafuatilia: 72
Idadi ya Twit alizoandika: 2,933
7. Ashton kutccher (@aplusk)

Kazi: Mcheza sinema na Mchekeshaji
Wanaomfuatilia: 6,827,108
Anaowafuatilia: 637
Idadi ya Twit alizoandika: 6,730
8. Ellen DeGeneres (@TheEllenShow)
Kazi: Mchekeshaji na Mwendesha kipindi cha televisheni cha mazungumzo
Wanaomfuatilia: 6,741,018
Anaowafuatilia: 48,480
Idadi ya Twit alizoandika: 4,498
9. Taylor Swift (@taylorswift13)
Kazi: Mwanamuziki
Wanaomfuatilia: 6,520,455
Anaowafuatilia: 55
Idadi ya Twit alizoandika: 942



10. Shakira (@shakira)


Kazi: Mwanamuziki

Wanaomfuatilia: 6,227,056
Anaowafuatilia: 39
Idadi ya Twit alizoandika: 989

>Motorola Atirx: Ni Simu na Kompyuta?

>

Motorola Atrix pamoja na lapdoki yake ambayo huiwezesha simu hii kuwa kama laptop
Motorola Atrix si simu inayotegemewa kuwa bora kuliko zote Duniani. Atrix imekuwa madukani kwa muda wa miezi 5 sasa, ingawa simu hii haijapata umaarufu mkubwa lakini ina sifa moja ya kipekee, huuzwa na gajet mbili muhimu nazo ni lapdoki (laptock) na multimedia dock. Lapdoki inapoungishwa na Atrix humuwezesha mtumiaji kuitumia simu yake kama kwamba ni laptop. Vile vile unaweza kununua Atrix pamoja na kibodi yake na maltimidia doki pamoja na skrini ya komyuta na kuifanya simu hiyo kuwa ni kompyuta ya deski. 

Jee inawezekana kuifanya simu hii kuwa ndio laptop au yako na hivyo kupunguza gharama za maisha ya kununua gajet mbili mbali mbali? Tutachambua namna ya lapdoki na doki za Atrix zinavyokuwezesha kuitumia simu hii kama kompyuta pamoja na mapungufu yake. 
Vianisho halisi
Kamera: Full HD 1080p, ni kamera ya kweli yenye uwezo wa hali ya juu. Pia ina megapiksel 5 kwa kamera ya nyuma na webcam kwa mbele.
Prosesa: Dual-core 1GHz ARM Cortex-A9 proccessor, ULP GeForce GPU, Tegra 2 chipset, prosesa hii ina nguvu za kutosha kuendesha hata laptop kamili.
Skrini: 4.0 aina ya capacitive. Ina pikseli za rezolushan 540×960. Hii inaifanya simu hii kuwa na skrini inayon’gara  na yenye kuonesha picha safi. Motorola wanaiita skrini hii qHD ambapo inakaribiana sana na skrini ya iPhone 4 yenye pikseli za rezolushan 640X960.

Kisoma alama za vidole katika Motorola Atrix
Alama za Vidole: Ina teknolojia ya biometric fingerprint ambayo humuwezesha mtumiaji kufunga na kufungua simu yake kwa kutumia alama za vidole. Hutumia vidole vaa pili baada ya gumba, vya mikono yote miwili ambapo mtumiaji hutakiwa kutengeneza alama za vidole kwa kusugua kwenye kisoma alama za vidole.
Motoblur: Motorola kama zilivyo kampuni nyingine zinazotumia Android kama OS ya simu zao, wameivalisha koti ambalo wameliita Motoblur (mfano HTC Sense katika simu za HTC) Motoblur imeifanya simu hii ivutie iweze kuleta mvuto wa aina yake tofauti na Android za kawaida. Motoblur pia ina wijeti (widgets) nyingi zinazoipamba na kuifanya yenye urahisi zaidi katika matumizi.
Atrix na vikorokoro vyake
Mengine: GPS, Digital Compass, HDMI port.

Vikorokoro: Mbali na doki, simu hii pia ina vikorokoro mbali mbali kama vile mouse yake pamoja na rimoti zote zinatumia blututh (bluetooth) 
OS: Android 2.2 Froyo, pia Motorola wametangaza kwamba wako jikoni wakiipika Android Gingerbread 2.3.3 hivyo tutegemee uboreshwaji wa OS ya simu hii hivi karibuni.
Apps: Baadhi ya apps muhimu ambazo zitakuwezesha kuitumia simu hii kama kompyuta na vile vile kuifanya simu hiyo ni yenye matumizi mengi ni. 
Google Search, Maps, Gmail, YouTube, Google Talk
Imewekwa Facebook, Twitter, MySpace kwenye app moja kwa hiyo katika mambo ya mitandao bashasha (social networks) simu hii haiko nyuma
Photo viewer/editor
Organizer
Quickoffice v3.0  ambayo ina document editor 
Adobe Flash 10.1 
Wijeti za Motoblur 
Pia tusisahau kuwa mbali na hizo tutakazozitaja pia kuna apps zaidi lya 150,000 katika soko la apps la Android (Android Market)
Je Motorola Atrix inaweza kuwa kompyuta mbadala?
Hili ndiyo suali la msingi katika makala hii. Hakuna jibu moja kwa vile ndio au hapana inategemea aina ya matumizi anayoyafanya mtumiaji.
Mambo ambayo Motorola Atrix kama kompyuta inaweza kuyafanya ni: 
Kuandika na kusoma email pamoja kusafu mtandao (surfing internet)
Kutengeneza na kuonesha dokumenti za aina ya word, spreadshit na hata presentation za kawaida zisizo na mambo mengi makubwa.
Kutazama picha, kusikiliza muziki, video, youtube pamoja na mambo yote ya multimedia bila ya matatizo yoyote.
Mitandao Bashasha: Facebook, Twitter, Myspace na kadhalika huweza kutumika kwa ubora wa hali ya juu.
Vikwazo
Ukiwa utatumia Atrix kama kompyuta, utakosa programmu zenye kufanya kazi kubwa  ambazo hupatikana kwenye Windows au MAc OSX. Apps za android nyingi hufanya kazi moja tena ndogo ndogo. Kwa mfano video editing si kazi ambayo utategemea kuifanya kwenye Kompyuta hii. 
Vile vile usitegemee ufanishi kama ule unaopatikana kwenye kompyuta halisi. 
Hata hivyo iwapo unataka kuifaidi simu yako zaidi basi Atrix na vikorokoro vyake itakuwezesha kufanya hivyo. BAdo pamoja na udhaifu wake kama kompyuta Atrix ni simu ya aina ya kipeke mpaka sasa.
Kwa hiyo basi , ikiwa wewe ni mtumiaji wa kompyuta kwa matumizi mado madogo kama vile kutembea mtandaoni, kuandika na kusoma email, kucheza game, kusikiliza muziki, video  nakuangalia picha, kuandika dokumenti zisizokilombwezwa sana basi Atrix inaweza kuwa ni kompyuta tosha kwako. 
Lakini ukiwa ni mtumiaji mwenye mambo mengi makubwa kama vile kutengeza video, kutengeneza website, kuhifadhi mafaili mengi mno, yaani magigabayti kwa magigabayti hadi matetrabayti, basi simu hii haikutoshi kuwa ni kompyuta kwako.

>Ushindani kati OS za Simu wapamba moto

>

Windows Phone kwenye embe boribo


Ikionekana kama ni kujibu mapigo ya Apple ambao wametangaza kuwa idadi ya apps katika soko lao imefikia nusu milioni, Google nao wametoa takwimu kwamba simu 350,000 za Android kwa siku huuzwa Duniani kote, tunaomba kusisitiza kuwa haya ni mauzo ya siku moja. Hii maana yake ni kwamba kwa wastani kila sekunde kuna watu wanne wananunua simu za Android pahala fulani Duniani. Kwa mwaka mmoja simu zipatazo milioni 127 za Android huuzwa Duniani kote. 


Mbali na takwimu hii Google wameshusha bomu jingine kwamba mpaka sasa soko la Android limeshauza apps bilioni 3. Hii nayo takwimu ambayo itawaumiza vichwa wapinzani na hasa Apple ambao wanalengo la kuwa na ukiritimba katika masoko kama haya, lakini Google wanaonekana kwenda sambamba nao. Hata hivyo apps nyingi katika soko hilo ni za bure hivyo hii haina maana ya kufasiriwa kifedha.
Hata hivyo ni lazima tukumbuke kwamba Apple hutoa simu moja tu kwa mwaka (ingawa mwaka huu kuna fununu kwamba Apple watatoa simu mbili, iPhone 5 na iPhone Nano) wa kati kuna watengenezaji wengi tu wa simu za Android, kampuni kubwa ikiwa ni Samsung, HTC, Sony Erricson, Motorola na LG. Kampuni zote hizi hutoa simu nyingi tu kila mwaka na zote zimo kwenye ushindani na simu moja kwa mwaka  kutoka Apple.
iOS na Android si wachezaji pekee katika uwanja huu. Windows phone kwa sasa inaonekana kushika namba 3, wiki hii nao wametangaza kwamba wataboresha OS ya simu zao kwa kuiambatanisha na huduma ya Mango. Mango itaingiza katika simu hizo mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na Facebook Chat, Office 365 pamoja na SkyDrive. Japokuwa hii itaziwezesha simu za Windows kutoa ufanisi zaidi katika kwa namna itakavyoambatanisha huduma mbali mbali kwa mtinndo wa hub ambao ndio simu hizi unatumia, makampuni na mashiriki ambayo yangependa kutumia simu hizi kwa shughuli za kikazi bado kwao si habari njema kwani Windows phone bado haina encryption na pia inakosa exchange activesync iliyokamilika. 
Uambatanishwaji wa Mango katika Simu za Windows pamoja na uboreshwaji wake utazifanya simu hizo kuwa na huduma mpya zipatazo 500, ni wazi kwamba karibu watu watapata wazimu kwa simu iwapo wataziendekeza mno, kwani utamaliza wiki bila ya kumaliza kuyafanya yale ambayo simu yako ina uwezo wa kuyafanya.
Nokia wao hivi karibuni wametangaza kuachana na soko lao la Apps lijulikanalo kama Ovi, kwa kifupi Nokia wamekubali kushindwa na sasa wameamua kujiunga na kambi ya Windows Phone. Kampuni hiyo inatarajiwa kuanza kutoa Simu za Windows mwishoni mwa mwaka huu. Nokia wanaonekana kuchelewa mno kwa vile wao ndio wa mwisho kuidampu Symbian, hii maana yake ni kwamba Symbian OS ambayo imetamba katika miaka ya tisini sasa inaingia kaburini. Ilale mahala pema OS ya Symbian. 

>Appstore yafikisha Apps Nusu Milioni!

>

Appstore yenyewe ni App 
katika iPad, iPod na iPhone

Duka la kuuzia programu za iPad, iPhone na iPod touch lijulikanalo kama Appstore limefikisha apps laki tano zilizosajiliwa. Taarifa hii imekuja huku wauza program wengine wakiwa na taabu ya kupata idadi ya kutosha ya Apps hasa RIM wanaotengezeza simu na tablet za Blackberry. Duka hi lilifunguliwa mwaka 2007 Apple walipotoa iPhone ya mwanzo kabisa. Apps ni kifupi cha application, hizi ni software ndogo ndogo ambazo hufanya kazi maalum.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kampuni ya Apple ukiondoa apps ambazo zimefutwa, zilizoachwa kuendelezwa na watengenezaji wao, zilizopigwa marufuku kwa kuvunja masharti ya Apple na zilizojitoa kwa kushindwa kutokana na ushindani mkubwa soko hilo linabakiwa na apps 400,000  ambazo ni sawa na 80% ya apps zote zilizosajiliwa.
Mmiliki wa iPhone, iPod Touch au iPad kuweza kununua apps zote hizi itagharimu $891,982.24 za kimarekani sawa na TSh 1,927,098,880.00 na utahitaji disk yenye ukubwa wa tetrabayt 7.5, hii ni taarifa kwa uchambuzi tu kwani kwa sasa haiwezekani kutengeneza simu au tablet ya namna hii, na kama itatengenezwa huenda ikagharimu bei kubwa kuliko bei ya apps zote tuliyoitaja hapo juu. La msingi zaidi ni kwamba kila utakachofikiria kwamba ungetaka simu, ipod au tablet yako ifanye basi kuna app yake. Hata hivyo Apple wana udhibiti mkubwa katika mambo ya ngono na imewahi kufuta app kadhaa katika masuala hayo. Uamuzi huu ulionekana kuwa ni wa busara kwani wamiliki wa iPod, iPad na iPhone ni wa rika zote, ikiwa n i pamoja na watoto.
Soko hili la apps limewatajirisha watengenezaji wa apps (developers) wengi tu. Unaposajili app kwa Apple kila app inaponunuliwa mtengezaji hupata 70% na Apple wanachukua asilimia 30%. App zinaanzia  bei $1.00 na nyingi huuzwa chini ya $5.00 za kimarekani, hivyo wanunuzi nao hufaidika kwa bei hizi nafuu, vile vile kuna apps nyingi ambazo ni za bure. 
App ya Market kwa ajili ya
simu na Tablet za Android
Duka la apps la pili kwa kuwa na idadi kubwa ya apps ni Android Market linalomilikiwa na Google kwa ajili ya apps za tablet na simu za Android. Duka hilo kwa sasa limekwishasajili apps 300,000, hii ni taarifa isiyo rasmi, kwa taarifa rasmi idadi ya Apps katika Android market ni 200,000. 

Wengi wanatabiri kwamba katika kipindi cha miaka isiyozidi miwili upo uwezekano wa Android kuwa na apps nyingi kuliko zile za Appstore. Hii inatokana na ukweli kwamba Android ni open source kwa hiyo hakuna udhibiti wala masharti mengi na magumu katika kuweza kusajili app. Matokeo yake ni kwamba app nyingi za Android ni za kiwango cha chini. 
RIM bado wana kasi ya chini, ili kuwahamasisha developers kujiunga na soko lao watengenezaji hawa wa simu na tablet za Blackberry wametoa changamoto kwa yoyote atakayesajili na kukubaliwa app yake katika soko hili basi atapata zawadi ya tablet, Blackberry Playbook bure. Kwa sasa Blackberry App World ina Apps chini ya 20,000 ambayo ni sawa na 5% ya Appstore. Blackberry hawana budi kukaza kamba.

>Kwa Nini Blackberry Haziingii Kwenye 10 Bora?

>

Nembo ya Blackberry simu maarufu kutokana na BBM

Kumi bora mara nyingi huwa ni mtazamo binafsi wa mwandishi au kundi fulani, hata hivyo ukiangalia chati za simu kumi bora mbali mbali zenye kutofautiana, kuna kitu kimoja zinafanana, nacho ni hakuna simu za Blackbery. Kwenye makala hii tutajaribu kufanya uchambuzi wa kina juu ya sababu zinazopelekea simu hizo kutokuwemo kwenye chati.



Blackberry ni simu zilizopata umaarufu mkubwa na kutumiwa na wateja wengi Duniani. Simu hizo hutengenezwa na kampuni iliyopata mafanikio katika sekta hii ijulikanayo kama Research In Motion maarufu zaidi kwa ufupisho wake, RIM. Pamoja na umaarufu wa simu hizo ni mara chache sana kuona simu za Blackberry zinaingia kwenye chati ya simu 10 bora. Kwa mfano tangu mwaka 2010 hadi sasa ni Blackberry Torch pekee ndiyo iliyoingia katika chati hiyo ambao inatawaliwa na simu za Apple, HTC na Samsung. Hata Blackberry Torch ilikaa kwa muda mchache na kutolewa.
RIM, nembo ya kampuni inayotengeneza simu za
Blackberry, Research In Motion
Ubora wa Blackberry
BBM: Simu hizi zimejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuwa na njia ya kutumiana ujumbe baina watumiaji wake ijulikanayo kama Blackberry Messenger (BBM) ambapo wateja hupeana Blackberry Pin (BBP) na kuweza kuwekana katika orodha ya wenye kutumiana ujumbe, vile vile mtumiaji anaweza kumuingiza mtumiaji mwenziwe katika BBM kwa ku-scan barcode yake iliyoko kwenye simu hizo. BBM imesababisha simu za RIM kupata umaarufu mkubwa miongoni mwa vija wa rika kati ya miaka 15 – 40 ukizingatia kwamba tumo kwenye wakati ambao mitandao ya kijamii au kibashasha (social network) ni kivutio kikubwa.
QWERTY kibodi: Hii inaendena sana na BBM kwa vile wengi wa watumiaji wa Blackberry huwa ni waandishi zaidi kuliko wazungumzaji katika simu zao, kibodi huwasaidia kuandika kwa kasi na urahisi kutokana na ufanisi mkubwa uliotumika na RIM kuzibuni (design) kibodi hizo.
Usalama (Security): Vile vile simu hizo zina usalama wa hali ya juu kwani si rahisi kwa mapaparazi, wapelelezi  au mahaka (hackers) kuweza kupata ujumbe kwa njia ya wizi kwa vile Blackberry inatumia mitandao yao wenyewe kama njia za kupeleka ujumbe. Hata imefikia baadhi ya serikali kutaka kupiga marufuku simu hizo kwani hata vyombo vya usalama vya nchi vilishindwa kupata kusoma BBM za watu wakihofia kwamba magaidi watatumia uchochoro huu kuweza kuwasiliana na hivyo kuhatarisha usalama wa nchi zao. Hii imeplekea watu wenye usiri kuvutiwa sana na simu hizo ikiwa ni pamoja na wanasiasa, wasanii na ‘masupastaa pamoja na maselebriti’ wengine.
QNX OS: Blackberry inatumia OS zao wenyewe ambazo hutumia utaratibu wa QNX. OS hii ina uwezo mkubwa wa kufanya mambo mengi sambamba (multi tasking) kwa namna ya kipekee, pia ina ufanisi wa hali ya juu kwa namna inavyofanya kazi. Muhimu zaidi ni kwamba Blackberry OS haihitaji kifaa (hardware) chenye kasi sana kufanya kazi kwa kasi, kwani OS hii ni nyepesi (lightiweight) mno.
Maradhi (Addiction): Utafiti unaonesha kwamba watumiaji wengi (si wote) wa Blackberry wana maradhi na simu zao kwa kuzitumia zaidi kuliko watumiaji wa simu nyingine zozote. Ukianza kutumia simu hizi basi ni taabu kuziacha, hali hii inachangiwa zaidi na BBM ambapo wengi wanapoitumia utadhani akili zimewaruka huwa hawasikii wala hawasikilizi, hucheka pekee yao na hujihisi hawako wapweke. Kwa upande wa RIM hili ni zuri kwani inakuwa si rahisi kumpoteza mteja.
Sehemu ya juu ya Blackberry Pearl 3G, ikionesha kamera yake
Udhaifu wa Blackberry
Zifuatazo ndio sababu za msingi zinazozifanya simu za blackberry kutokuwemo katika chati ya simu bora Duniani pamoja na kuwa na ubora tulioueleza mwanzoni:- 
Skrini: Kwa asili simu za Balckberry zina skrini ndogo ukifananisha na simu ambazo hutamba kwenye kumi bora. Simu zote zilizokuwa kwenye kumi bora kwa sasa zina ukubwa wa skrini  baina ya inchi 3.5 na 4.3. Bila ya shaka kampuni ya RIM wanalifahamu hilo ndio maana wakajaribu kutengeneza simu kama vile Torch na Storm. 
Ubora wa Skrini (Quality): Rizolushan (Resolution) ni za hali ya chini kwa mfano Blackberry curve ina rizolushan 320X240, hii husababisha simu za Blackberry kutokuwa na mvuto wala mng’aro kwenye skirni kama zilivyo simu ambazo zinakuwemo kwenye kumi bora. Itakuwa si sahihi kulinganisha iPhone 4 na Curve kwa hiyo hebu tuangalie iPhone 4 ambyo ndiyo simu inayoweka viwango na Torch. iPhone 4 ina rizolishan 960X640 na PPI (pixel per inch) 326. na BB Torch ina rizolushan 480X360 na PPI 187.5, kwa mapana na maferu tunaweza kusema kwamba hii ni aibu kwa RIM. Skrini huchukuliwa kuwa ni hali ya juu (high end) ikiwa na PPI 300 na ya hali ya chini (low quality) ikiwa na PPI 150 au pungufu. Hii itakupa picha ni vipi Blackberry wanabana matumizi katika masuala ya Skrini.
Bofa Skrini: Wakati simu za skrini za kugusa (touch screen) zinaingia na kupata umaarufu kuanzia miaka ya 2007 ilipotoka iPhone, RIM wakataka kujitofautisha na kutoa skrini za kubofa (click screen) badala ya kugusa, hii iliwaangusha vibaya kwani simu hizo hazikuweza kukubalika na wateja, athari yake katika makosa kama haya yamepelekea jina la Blackberry na RIM (brand name) kushuka thamani kwa 20%, (Chanzo WPP). Sasa linganisha na Apple watengezaji wa iPhone  ambapo brand yao imekuwa kwa 84% (Chanzo WPP)
Umbile: Nadhani hata baadhi ya watumiaji wa Blackberry watakiri kwamba simu hizi hazina maumbile ya kuvutia ukilinganisha na simu za Samsung, Apple, LG, Sony Ercisson na HTC. Hii imechangiwa zaidi na utaratibu wa RIM kuwa ni muhimu kwao kuweka QWERTY kibodi. Iwapo RIM wanataka kutoa ushindani katika simu za hali ya juu basi hawana budi kuwafukuza kazi baadhi ya wabunifu wa maumbile (designers) wao na kuajiri wapya.
Vianisho Halisi (Specs): Hapa hatuna maelezo mengi tutalinganisha Blakberry bora kuliko zote kwa viainisho (Torch) na Samsung Galaxy Ace ambayo ndiyo ya mwisho katika kumi bora za mwezi huu:
Torch: CPU 624 MHz, Kamera 5 mp, Video VGA 24 fps, Betri masaa 5:40 (kuzungumza), RAM 512.
Ace: CPU 800 Mhz, Kamera 5MP, Video VGA 15 fps, Betri masaa 6:30 (kuzungumza) RAM 256.
Kwa hiyo Torch inaikaribia simu ya mwisho kabisa katika kumi bora, iwapo wanataka kuingia katika simu bora hawana budi kuwa na viainisho halisi bora zaidi ili kutoa ushindani wa kweli.
Blackberry App World: hii ni aibu ya pili kwa RIM, soko hili la apps lina apps zisizozidi 20,000 ambapo ni chini ya 10% ya appstore ya Apple yenye  apps zaidi ya 200,000 na Android Market yenye apps zaidi ya 150,000. RIM wanalifahamu hili, katika kufanya juhudi za kuwahamasisha watengenezaji wa apps kuingia kwenye soko lao RIM wametoa ahadi ya kumpa zawadi yoyote atakayepeleka app yake kwenye soko lao na kupasishwa, ambapo zawadi yenyewe ni Blackberry Playbook tablet ya bure.
Ni matumaini ya washabiki wa Blackberry na wapenda gajet Ulimwenguni kuwa RIM wamepata funzo kubwa kwenye utengezaji wao wa Blackberry Playbook na udhaifu uliowazi wa simu za Blackaberry. Playbook ni tablet ambayo inatarajiwa kupata mafanikio kwa kuwa imetengenezwa kwa umahiri mkubwa. 


Sisi katika Gajetek tunaamini kwamba  simu ya Blackberry ijayo itaingia katika cha chati yetu ya simu na kukaa kwa muda mrefu. Hata hivyo RIM wafanye haraka kabla ya Blackberry haijageuka kuwa Crapberry.

>Simu: Kumi Bora (Sehemu 1)

>

1. Samsung Galaxy S 2 
Samsung Galaxy SII
Kinachoifanya simu hii kuwa kileleni kwenye chati ni ubora wa vianisho halisi vyake, ina kasi na nguvu na pia ni simu nyebamba kuliko zote Duniani ambapo imeipiku iPhone 4 katika sifa hii. Ina kamera nzuri, yenye kutoa picha safi mno na uwezo wa kurekodi video za HD, vifuatavyo ni vianisho halisi vyake:-



Video: Full HD 1080p na megapiksel, ukiwa na simu hii basi huhitaji kamkoda wala kamera, simu nyingi kamera zake ni maskhara tu, lakini Galaxy S2 si hivyo ni kamera ya kweli yenye uwezo wa hali ya juu. Bila ya kutia chumvi unaweza hata kurekodi harusi iwapo utapata mwangaza wa kutosha.


Prosesa: Dual Core 1.2 Ghz aina ya snapdragon, hii ni prosesa yenye nguvu za kuendesha hata laptop wacha kijisimu, ina kasi kiasi kupindukia kasi inayohitajika kwenye simu. 
Skrini: 4.3 Super Amoled Plus, hii inaifanya simu hii kuwa na skrini inayon’gara sana. Unaweza kutazama kwa pembe (angle) ya  chini kabisa na kuona kwa vizuri na bila ya matatizo.
Kamera: megapiksel nane yenye flashi inaifanya simu hii kuwa na kamera yenye ufanisi kuliko zote kwenye simu, zipo simu zinazofanana na simu hii kwenye piksel hizi lakini mpaka sasa hakuna zaidi yake.
Umbile: Ikiwa na wembamba wa milimita 8.49 inaifanya simu hii kuwa ni simu nyembamba kuliko zote Duniani. Vile vile simu hii ina uwezo wa kutuma ujumbe mfupi kwa sauti ikitumia teknolojia ya Google ya kutambua sauti (voice recognition) na pia inatumia Android Gingerbread 2.3 ambayo ni toleo jipya la OS ya Android kwenye simu.
Simu hii imekamata kilele katika chati ya simu mwezi huu kwa kuipiku iPhone 4, je simu hii itaweza kubaki kileleni itakapotolewa iPhone 5 baina ya mwezi wa Juni na Septemba mwaka huu? Hatuna jibu, ni vyema tu tusubiri.
2. iPhone 4
iPhone 4 nyeupe
Simu hii imekuwa kilele kwa muda wa zaidi ya miezi kumi, kutokana na wingi wa simu na namna simu zinavyobadilika haraka si rahisi kwa simu kuwa kwenye chati kwa zaidi ya mwezi mmoja, hii inathibitisha namna ambavyo simu hii ilizitangulia simu nyingine kwa wakati ilipotolewa. Yavutayo ndio yanaifhanya simu huu kuwa ni miongoni mwa si bora:
OS: iOS 4.3.3 yenye ubora, ikitumia OS ambayo haipatikani kwenye simu yoyote nyingine, inaifanya iPhone kukosa ushindani wa karibu kwenye nukta hii. OS hii ni rahisi kuitumia na ina ufanisi bora.
Appstore: Hili ni duka la kununulia apps (program), lina apps zaidi ya laki mbili, ni kweli kabisa kama Apple wanavyodai kwenye tangazo la simu hii “kama huna iPhone basi huna iPhone” Karibu kila unachofikiria ambacho ungependa simu yako ifanye basi kuna app yake kwenye duka hili.
Skrini: Skrini yake ambayo inaitwa Retina inaukubwa wa inchi 3.5 na piksel kwa kila inchi (ppi) ni 320. Uwezo wa jicho kuona ni mwisho ppi 300 unapikamata kitu kiasi cha umbali wa sentimita 25 hivi. Hii maana yake ni kwamba macho yetu hayana uwezo wa kuona uzuri wa skrini ya iphone, yaani ni nzuri kuliko tunavyoiona.
SSD: Huhitaji kukunua SD kadi kwani haitumii teknolojia hiyo. Hata hivyo ina disk aina ya SSD (solid State Disk) yenye ukubwa baina ya 16GB na 32GB. Apple wanadai kwamba kadi za SD hupnguza kasi za simu.
iTunes: Mawasiliano baina ya simu hii na kompyuta hufanywa kwa kutumia program ya  iTunes, hii hurahisisha kazi ya ku-backup simu na kuingiza mafaili kama vile muziki, vitabu (E Books), picha, video na apps na pia kuhamisha video, picha na apps zilizo kwenye i`phone kwenda kwenye kompyuta kwa ajili ya kutumia au kuhifadhi.
Umbile: Simu hii ina umbile la kipekee, ambapo ina kioo mbele na nyumba, ni ya pili kwa wembamba baada ya Samsung Galaxy S2 ambapo ina wembamba wa milimita 9.3 na ina kona za kiduara zinazoifanya kukamatika kuwe ni rahisi . 

3. HTC Sensation 

HTC Sensation

Huwezi kuzungumzia simu bora bila ya kuitaja HTC. Sensation kama jina lake ni simu ambayo ina ufanisi usiojificha.
Kuzima mlio: Simu hii kama zilivyo baadhi ya HTC, inapoita na ukaichukua na kuifunika kwa kuigeuza skrini kuelekea chini basi hunyamaza, ukiwa mkutanoni au darasani na umesahau kuitoa sauti basi hii teknolojia itakufaa sana wakati huo.
Vianisho halisi: Simu hii inafanana mambo mengi na Galaxy 2 ikiwa ni pamoja na Android Gingerbread ,  kamera yenye megapiksel nane,  prosesa aina ya dula core yenye kasi ya 1.2 Ghz na ndio maana ipo karibu na juu kwenye chati hii. 
Skrini: Ikiwa na ukubwa wa inchi 4.3 yenye mn’garo ulikithiri, uzuri skrini hii haitofautiani sana na skrini ya Samsung Galaxy S2.
HTC Sense: simu hii pia imevalishwa koti ya HTC Sense ambapo linaweza kukufanya usahau kama unatumia Android kwa namna koti hili lilivyo la kipekee. HTC Sense inaonyesha habari muhimu kwa urahisi ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, saa na tarehe katika mji uliopo, unaposafiri basi HTC Sense kwa kutumia sensa za GPS nayo hubadilika wenyewe kwa mujibu wa mji uliopo
HTC Sync: HTC sensation pia hutumia HTC Sync kuhamisha mafaili baina yake na kompyuta na hivyo kuifanya kazi hii kuwa ni rahisi kwa kiasi fulani tofauti na chukua na weka (drg and drop) inayotumika kwenye simu nyingine.

Umbile: Simu hii pia ina upana wa milimita 11 pana kwa milimita 2 tu ukifanannisha na iPhone bado inapendeza kwa kuiona na kuishika mkononi ni rahisi. Pia gamba lake limetengeneswa kwa namna ambayo HTC wenye we wanaiita ‘unibody’ yaani halina kufungwa msumari wala kuunganishwa unganishwa.

4. Motorola Atrix Laptop
Motorola Atrix
Simu hii ni moto kama ulivyo uhamasishaji wa Motorola ‘Moto’. Motorola wanastahiki kupengezwa kwa uvumbuzi wa kisasa walioufanya kwenye Atrix. 
Dock: Doki hii hujulikana kama HD multimedia dock. Hichi kifaa ambacho unaiweka simu hii hukuwezesha kutumia internet ya simu kwenye kompyuta yako. Doki hii inakuwezesha kuunganisha simu hii na TV, kompyuta, skrini, mouse na keyboard kwa kutumia USB na HDMI.
Lapdock: Pia Atrix ina kifaa kijulikanacho kama Lapdock. Hii huigeuza Atrix kuwa laptop kamili. kila kilichomo kwenye simu inapokwa simu hii kwenye lapdock huwa kinaweza kupatikana kwenye lapdock ikiwa ni pamoja na mtandao wa simu, mafaili ya picha, muziki au video yaliyopo kwenye simu. Pia lapdock hii inauwezo ya kuonesha HD. 
Lapdock na Atrix ikiwa imepachikwa

Vianisho halisi: Simu hii pia ni Android ambayo ilipotoka ilitumia toleo la Froyo 2.2 lakini kwa sasa unaweza kuiboresha na kuweka Android 2.3 Gingerbread. ina kamera yenye megapiksel 5.

Fingerprint: Simu hii ina usalama mkubwa. Ina teknolojia ya fingerprint inayokuwezesha kuitia loki na hivyo ni aliyeifunga tu kwa kutumia vidole ndiye utakaeweza kuifungua. Huna haja ya kukumbuka neno lasiri (password) wala kuwa na wasi wasi wa mtu wa karibu yako kuweza kujua neno la siri unalotumia
Hivyo badala ya kununua laptop na Simu waweza kununua Motorola Atrix na lapdock yake, ikiwa unataka kutumia kwa ajili ya kujifurahisha kwa video, muziki na picha basi dock maalum kwa shughuli hii (entertainment dock) hakitkufanya ujihisi kwamba umepungukiwa.
Sehemu ya pili ya makala hii tutazielezea simu zenye kushika nafasi ya sita hadi ya kumi nazo ni:
Sony Ericsson Xperia Arc
Google Nexus S 
LG Optimus 2X 
HTC Desire S
HTC Incredible S
Samsung Galaxy S